• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
Umaskini wasukuma wavuvi bahari hatari

Umaskini wasukuma wavuvi bahari hatari

Na KALUME KAZUNGU

WAVUVI katika Kaunti ya Lamu wanaendelea kuhatarisha maisha yao baharini kwa sababu ya umasikini, licha ya serikali kuwaonya mara kadhaa kuhusu msimu wa mawimbi makali.

Katika siku za hivi majuzi, Lamu imeshuhudia ajali nyingi za mashua za wavuvi, ambapo wengi wameishia kujeruhiwa au kufariki baada ya mashua zao kuzama wakati wakitekeleza uvuvi baharini.

Katika kipindi cha juma moja lililopita pekee, kumekuwa na karibu ajali tano za mashua za wavuvi baharini.

Wavuvi waliohojiwa na Taifa Leo walisema kuwa hawana namna nyingine kujipatia riziki kwa hivyo inawalazimu kuingia bahari hata nyakati zisizofaa ili kukimu mahitaji ya familia zao.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Kusimamia Wavuvi (BMU) kisiwani Lamu, Bw Abubakar Twalib, alisema wao huonelea heri wafe wakitafutia familia zao badala ya kusubiri hadi hali shwari kujiri.

“Licha ya kukatazwa kuingia baharini misimu kama hii, mvuvi wa Lamu hana budi ila kuhatarisha maisha yake akitafuta siku zote. Yote yanatokana na umaskini,” akasema Bw Twalib ambaye amedumu kwenye sekta ya uvuvi kwa miaka 12.

Mnamo Jumatatu, wavuvi watatu, Shee Mohammed, Fuad Mohamed na Ali Mohammed walinusurika kifo pale mashua yao iliposombwa na mawimbi ikazama eneo la Mlango wa Shella.

Ijumaa wiki iliyopita, wavuvi wanne, Shee Issa, Arafat Titi, Mahmoud Mohamed na Mohamed Dili walinusurika kifo kwa kuogelea kwa zaidi ya saa sita kabla ya kukumbatia jiwe baharini baada ya boti yao kuzama eneo la Ziwani karibu na Kiunga, Lamu Mashariki.

Wavuvi wawili waliotoweka majuma mawili yaliyopita baada ya mashua yao kuzama baharini eneo la Tenewi, Kaunti ya Lamu bado hawajulikani waliko.

Walikuwa miongoni mwa wavuvi watano waliosafiri kutoka Ngomeni, kaunti ya Kilifi kuja Lamu kwa shughuli za uvuvi. Watatu waliokolewa.

Mapema mwezi huu Agosti, wavuvi watatu, Aboud Obbo, Mohamed Obbo na Aboud Mzee waliokolewa mashua yao ilipozama eneo la Pezali karibu na kisiwa cha Shanga-Rubu huko Lamu Mashariki.

Julai 2021, mabaharia saba kutoka Tanzania waliokolewa na Navy wakati boti yao iliposombwa na mawimbi makali na kuzama eneo la Shanga, kaunti ya Lamu.

Saba hao walikuwa wametoka Dar es Salaam, Tanzania kuelekea Kismayu nchini Somalia kabla ya ajali hiyo kutokea Lamu.

Mkurugenzi wa hali ya anga katika kaunti hiyo, Bw Edward Ngure, alisema ofisi yake imefanya kila jitihada kutoa tahadhari za mara kwa mara kwa wavuvi na mabaharia wengine dhidi ya kusafiri baharini nyakati za dhoruba.

“Nimejaribu hata kuunda makundi ya mtandao, ikiwemo WhatsApp ili kusambaza jumbe kuhusu hali ya anga na usafiri wa baharini ili kuepuka ajali. Ni vyema tuheshimu maonyo hayo kwa manufaa yetu,” akasema Bw Ngure.

Katibu wa BMU Lamu, Mohamed Somo alilalamika kuwa, miradi mikubwa ya serikali kama vile ujenzi wa bandari uliharibu maegesho yao na kuongeza michanga sehemu nyingine za bahari walizotegemea kwa uvuvi, ilhali hawajalipwa fidia hadi leo.

“Sehemu ambazo hufanikisha shughuli zetu sasa ni zilizo katika maji makuu baharini. Bahari ikichafuka sehemu hizi huwa hatari. Ombi letu ni serikali kutuzingatia na kutufidia ili tuangazie biashara nyingine zitakazotusaidia maishani,” akasema Bw Somo.

You can share this post!

Makala ya spoti – Nyika Queens FC ya Taita Taveta

Wakili ataka Jumwa amlipe Sh22.6m