• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Makala ya spoti – Nyika Queens FC ya Taita Taveta

Makala ya spoti – Nyika Queens FC ya Taita Taveta

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

NYIKA Queens FC ni mojawapo ya klabu zilizoathirika pakubwa kutokana na kusimamishwa kwa michezo sababu ya janga la corona.

Kutokana na kutocheza mechi za ligi kwa kipindi cha mwaka mmoja michezo ilipopigwa marufuku, timu hiyo ya Nyika Queens ilikuwa kati ya zile ambazo zilipoteza mwelekeo na ziko kwenye harakati za kutafuta mbinu za kurudisha hali nzuri ya wachezaji wao.

Nyika Queens FC iliyofufuliwa mwaka 2020 baada ya kutocheza kwa miaka mitatu, haikuweza kufua dafu kutokana na wachezaji wake kukaa bila ya kufanya mazoezi na wakitii amari ya makatazo yaliyotolewa na serikali ya kutojihusisha na michezo yoyote janga la Covid-19 lilipochipuka.

Mwanzilishi wa klabu hiyo, Twalha Mazambi anasema walipoanza kucheza mechi yao ya ufunguzi ya Ligi ya Soka la Wanawake ya Kunti ya Taita Taveta ya msimu huu dhidi ya Pema Ladies FC walichapwa mabao 8-0 kwa sababu hawakuwa wamejitayarisha vizuri.

“Tulikuwa hatukujitayarisha vizuri kwa sababu tulikuwa ndio mwanzo tunakusanya wasichana wetu ambao walikuwa safarini na hawakuwahi kufanya mazoezi ya kutosha ya kukabiliana na wapinzani wao waliokuwa uwanja wa nyumbani kwao Mwatate,” akasema Twalha.

Celina Malemba Masese…Nahodha wa Nyika Queens FC. PICHA/ABDULRAHMAN SHERIFF

Akiwa na mwanzilishi mwenzake Madam Saumu, Twalha anasema wamejikita na watafanya vizuri kwenye mechi zao nyingine kwani watapata fursa nzuri ya kujiandaa. “Tutajiandaa vya kutosha ili kwenye mechi zetu zijazo, tuweze kutamba,” akasema.

Kocha wa timu hiyo, Mustafa Mwangu amesema kikosi chake kingali kichanga mno lakini kila wachezaji watakapokuwa wakicheza mechi za kirafiki na ligi, wataweza kujifunza mengi na hivyo wataweza kucheza vizuri kwenye mechi zao zijazo.

“Naamini tutaanza kuonyesha makucha yetu katika mechi zitakazofanyika baadaye kwani hivi sasa wasichana wangu wanajifunza mbinu maridhawa za kukabiliana na wapinzani wao,” akasema Mwangu.

Kikosi cha timu yake hiyo ambacho kimekusanya wachezaji kutoka maeneo ya Msanganyika, Mambura na Mwachawaza kina Celina Malemba Masese (Nahodha), Catherine Maghanga, Agripinah Mwakilenge, Wakesho Kota, Oripa Samba na Prisca Mwaisaka.

Wanasoka wengine katika kikosi hicho ni Lizzie Mwawigwa, Jackline Mjomba, Evangeline Kinyika, Mary Wakesho, Florence Mzee, Hendrita Mwamboje, Fatuma Mghendi, Janet Wali, Hanifah Mwazo na Velice Mbogho.

Nahodha Celina Malemba Masese amesema wamepania kuhakikisha kama si msimu huu basi msimu ujao, watafanya bidii timu yao iwe mojawapo ya zile maarufu za soka la wanawake katika kaunti hiyo ya Taita Taveta.

“Kushindwa kwa mechi yetu ya kwanza msimu huu kumetupa somo kubwa ambalo tunataka kuhakikisha tunajirekebisha na tunafanya vizuri kwenye mechi zetu nyingine tutakazocheza msimu huu. Tumeanza kujipanga na kujitayarisha kwa mechi zijazo,” akasema Celina.

Mwanzilishi mwingine wa klabu hiyo, Madam Saumu amesema waliamua kuirudisha timu hiyo kiwanjani kwa sababu ya kuwasaidia wasichana wanaopenda kucheza soka wapate kuendeleza vipaji vya uchezaji wao ambavyo vinaweza kuwasaidia kufika mbali.

“Niliwaona wasichana wa sehemu yetu hii wakitaka kucheza kandanda na kuwa na nia kubwa ya kuendeleza vipaji vyao ili nao watambulike katika ramani ya soka ya nchini Kenya. Wana hamu nao kuichezea timu ya taifa ya Harambee Starlets,” akasema meneja huyo.

Alitoa ombi kwa wahisani wakiwemo wafanya biashara na viongozi wa siasa wajitokeze kuwadhamini ili waweze kuwapa fursa wasichana wao kucheza mechi za kirafiki dhidi ya kaunti nyingine za jimbo la Pwani kwa matayarisho ya mechi zao zijazo.

  • Tags

You can share this post!

Siraj apigania kupata namba Harambee Stars

Umaskini wasukuma wavuvi bahari hatari