• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
‘Ushirika wa ODM, Jubilee moto wa kuotea mbali’

‘Ushirika wa ODM, Jubilee moto wa kuotea mbali’

Na BENSON MATHEKA

VIONGOZI wa chama cha Jubilee, wametaja vyama vya ODM na Wiper, kama washirika wake muhimu na kupuuza madai ya Naibu Rais William Ruto kwamba kimesambaratika wakisema atashangaa hivi karibuni kitakapopata nguvu mpya.

Wanasema chama hicho kinaendelea kujipanga kwa kutia nguvu ushirikiano wake na vyama vingine vya kisiasa ambavyo vimeonyesha nia ya kufanya kazi nacho.Chama hicho kinasuka muungano na chama cha ODM, hatua ambayo imekosolewa na vyama vingine kikiwemo United Democratic Alliance (UDA) cha Naibu Rais William Ruto aliyetaja muungano huo kama wa kikabila.

Kulingana na katibu wa Jubilee bungeni, Aden Keynan, wanaosisitiza Jubilee imekufa watashangazwa na yatakayojiri kikikamilisha mikakati yake.Alisema chini ya Rais Uhuru Kenyatta, chama hicho kinaweka mikakati itakayotikisa siasa za Kenya uchaguzi mkuu unapokaribia.

Mikakati hiyo, alieleza, ni kuimarisha ushirikiano wake na vyama vingine akitaja ODM kinachoongozwa na Raila Odinga na Wiper cha aliyekuwa makamu wa rais Kalonzo Musyoka.’Raila Odinga sio kiongozi wa serikali lakini anaongoza chama chenye nguvu, Kalonzo sio mbunge lakini anaongoza chama muhimu sana.

Kwa kuzingatia haya, wale wanaodhani sababu muhula wa rais unakaribia kukamilika Jubilee itaisha, watashangaa,” alisema.Akizungumza kwenye kipindi kimoja cha runinga jana asubuhi, Bw Keynan alisema tangu mfumo wa siasa za vyama vingi nchini uanze, kila uchaguzi huwa tofauti huku miungano ikiibuka na hivi ndivyo Jubilee inavyofanya kwa wakati huu.

“Sisi kama Jubilee tunaimarisha ushirikiano tulio nao na ODM ndani na nje ya bunge chini ya handisheki kuwa muungano. Ni ushirikiano sawa na tuliokuwa na Wiper na vyama vingine vilivyo na msimamo sawa na wetu.

Kama Jubilee tumejitolea na tuko tayari,” alisema Bw Keynan.Muungano wa ODM na Jubilee unachukuliwa kuwa wa kumwandalia Bw Odinga njia ya kumrithi Rais Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu ujao ingawa waziri mkuu huyo wa zamani hajatangaza iwapo atagombea urais.

  • Tags

You can share this post!

Somalia, Afghanistan hatari zaidi kwa maisha ya watoto

Muturi aelekeze Mlima Kenya waseme kwa sauti moja