• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Ushuru: Wenye baa wamtaka Ruto aongee

Ushuru: Wenye baa wamtaka Ruto aongee

NA MARY WANGARI

WENYE vilabu na hoteli nchini sasa wanamtaka Naibu Rais, William Ruto kujitokeza na kufafanua wazi pendekezo linalopigiwa debe na Mbunge Kimani Ichung’wa kuhusu kuongezwa kwa ushuru wa pombe.

Kupitia muungano wao wa kitaifa wa Wafanyabiashara wa Baa na Hoteli Nchini (BAHLITA), wafanyabiashara hao wamepinga vikali mswada unaoungwa mkono na mbunge huyo wa Kikuyu, Kaunti ya Kiambu.

Endapo Mswada wa Fedha 2022 uliopendekezwa na Wizara ya Fedha utaidhinishwa kuwa sheria, ushuru mpya utaongezwa hadi asilimia 10 na asilimia 20 kwa pombe ya kawaida na ile ya vileo mtawalia.

Ushuru unaotozwa chupa za gilasi za kupakia pombe utaongezwa hadi asilimia 25 huku ushuru unaotozwa matangazo yanayohusu bidhaa za pombe ukiongezwa hadi asilimia 15.

Wanachama wa BAHLITA kutoka kaunti zote 42, kupitia mwenyekiti wao, Simon Njoroge, Alhamisi walimtaka Naibu Rais kueleza iwapo pendekezo la Bw Ichung’wa linawasilisha msimamo rasmi wa United Democratic Alliance (UDA).

“Tumepanga kuwa na kikao na Naibu Rais William Ruto ili atufafanulie ikiwa pendekezo la Mbunge Ichung’wa kuhusu kuongeza ushuru wa pombe ni msimamo wa UDA. Ikiwa UDA haiungi mkono mswada huo basi tunataka Ichung’wa achukuliwe hatua za kinidhamu. Tunatazama kwa makini kinachoendelea Bungeni kuhusu mswada huo. Sisi kama wawekezaji tumewaelekeza wanachama wetu wote. Hatuwezi kuwapa kura zetu wabunge wanaounga mkono nyongeza ya ushuru. Hatuwezi kuwapa kazi huku wakituharibia kazi,” alisema Bw Njoroge alipohutubia wanahabari katika Hoteli ya Sagret, Nairobi.

Bw Njoroge alilalamika kuwa, hatua ya kuongeza ushuru wa pombe itakuwa pigo kuu kwa sekta ya burudani ambayo iliathirika zaidi kutokana na janga la Covid-19.

Sekta ya burudani inakadiria hasara ya Sh19.8 bilioni kila mwaka huku idadi ya vilabu nchini ikipungua hadi 32,000 kutoka 54,000 na kusababisha waajiriwa wasiopungua 110,000 kupoteza kazi, kulingana na Mwenyekiti huyo.

Naibu Mwenyekiti wa BAHLITA, Charles Loidima Nasieko alihoji kuwa hatua ya kuongeza ushuru wa pombe halali, kando na kusababisha kuongezeka kwa pombe haramu zinazohatarisha afya, vilevile itawaadhiri wakulima wa shayiri na mtama zinazotumika kutengeza pombe.

  • Tags

You can share this post!

Biashara zaathirika katika kaunti fujo zinahofiwa kutokea

TAHARIRI: Tusifanyie suala la ardhi mchezo kama ilivyo sasa

T L