• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
TAHARIRI: Tusifanyie suala la ardhi mchezo kama ilivyo sasa

TAHARIRI: Tusifanyie suala la ardhi mchezo kama ilivyo sasa

NA MHARIRI

HUKU tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, wanasiasa wengi wamekuwa wakitoa ahadi nyingi watakazotimiza endapo wapigakura watawachagua kuwawakilisha kwenye nyadhifa mbalimbali.

Lakini cha kushangaza ni kuwa, Wakenya wengi huenda wakaingia kwenye mtego wa ahadi hizo na kuwachagua wanasiasa hao ila baadaye wakawa na majuto mengi kwa kipindi chote cha miaka mitano ijayo.

Cha kushangaza ni kuwa, wanasiasa hawa watatumia pesa kama chambo cha kuwanasa wapigakura maskini watakaoamini yote wanayoambiwa na hatimaye kuwapa kura zao.

Hata baada ya Kenya kujinyakulia uhuru zaidi ya miaka 50 iliyopita, inashangaza kuwa wanasiasa wangali wanatumia ulaghai kuwanasa wapigakura, badala ya kutumia uhalisia.

Suala la umaskini na ukosefu wa ajira ni sababu kuu zinazofanya raia wengi kuwaandama wanasiasa na kuwaabudu kama miungu kwa imani kuwa watabadili maisha yao.

Hicho kiwe kidokezo kwa wanasiasa watakaoshinda kura; wajitahidi kubuni nafasi nyingi za kazi iwezekanavyo kama njia ya kumaliza umaskini.

Hivyo basi, ni makosa kwa mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja-One Kenya kutumia suala hili kama chambo, maadamu mirengo hiyo yote ina watu waliowahi kutajwa katika sakata mbalimbali za ardhi.

Sote tunafahamu fika kuwa ghasia za mwaka 2007/08 zilichangiwa pakubwa na suala lili hili la ardhi ambapo Wakenya wengi waliaga dunia,maelfu kupoteza mali yao na wengine kuwa wakimbizi wa ndani kwa ndani nchini mwao.

Siasa za ardhi ni donda ndugu na zaweza kulitumbukiza taifa hili kwenye janga kuu, ikizingatiwa kuna maskwota wengi nchini.

Ingekuwa busara sana endapo ripoti mbili za awali – ile ya Jaji Ndun’gu maarufu kama Ndungu Report na ile ya Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano (NCIC) zingetumika kutatua utata wa ardhi nchini.

Anachosema Naibu Rais, Dkt William Ruto kuwa serikali yake itatenga pesa kununua ardhi kubwa zisizotumika ili kuwapa maskwota ni sawa ila hatuoni atakapotoa pesa hizo ikitiliwa maanani ahadi nyingi alizowaahidi Wakenya hadi sasa.

Kwa upande wake, Bw Raila Odinga anasema serikali yake itatwaa ardhi zote zilizonyakuliwa na kuwafidi maskwota. Huu ni mchezo mbaya na hatari sana kwani huenda ukaleta mzozo mkubwa kama ulioshuhudiwa nchini Zimbabwe katika hatamu ya marehemu Robert Mugabe alipojaribu kunyakua mashamba ya Wazungu kuwapa Waafrika.

Sote tunajua ujanja wa wanasiasa. Ahadi za kuwapa maskwota ardhi wakati huu wa kampeni ni hatari sana na zaweza kulitumbukiza taifa hili kwenye mzozo utakaovuruga amani ya nchi miaka mingi ijayo.

Wanasiasa wetu wachunge ndimi zao kwani mengi wanayosema sasa huenda yakaharibu utangamano wa nchi.

You can share this post!

Ushuru: Wenye baa wamtaka Ruto aongee

CECIL ODONGO: Ruto na Raila hawawezi kutatua jinamizi la...

T L