• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Uteuzi wa Chiloba ni njama ya kuboronga uchaguzi 2022 – Akombe

Uteuzi wa Chiloba ni njama ya kuboronga uchaguzi 2022 – Akombe

Na SAMMY WAWERU

ALIYEKUWA kamishna katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Dkt Roselyn Akombe  amedai uteuzi wa aliyekuwa afisa mkuu mtendaji wa tume hiyo Ezra Chiloba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano (CA) ni njama ya kuboronga matokeo ya uchaguzi mkuu ujao.

Jumanne jioni, muda mfupi baada ya CA kutuma taarifa kwa vyombo vya Habari kuhusu uteuzi wa Bw Chiloba, Akombe alichapisha madai hayo kwenye ukurasa wake wa Twitter.

“Kutoakana na uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu mpya wa CAK (akimaanisha CA), mchakato wa uchaguzi wa 2022 umepangwa vizuri,” @DrRoselyneAkombe akaelezea.

Akaongeza: “CAK – Usambazaji wa matokeo kieletroniki.”

Mamlaka ya Mawasiliano Nchini ilisema imemteua Bw Chiloba baada ya kufuzu kufuatia maombi ya waliomezea mate wadhifa huo iliotaja ulikuwa na ushindani mkuu.

Chiloba aliondolewa afisini na IEBC 2018 kwa kile tume hiyo ilidai alipatikana na makosa ya kukiuka mikakati ya utoaji zabuni katika uchaguzi mkuu wa 2017 na marudio ya urais.

Kufuatia uteuzi wa jana, atahudumu kipindi cha miaka minne mfululizo. Aidha, kipindi hicho kikikamilika, anaweza kuomba upya au kuteuliwa kuendelea kuhudumu kwa awamu nyingine.

Dkt Akombe alijiuzulu Oktoba 18, 2017, siku nane kabla ya marudio ya uchaguzi wa kiti cha urais akidai alichukua hatua hiyo “kwa sababu zoezi hilo halitakuwa la huru, haki na wazi”.

Bw Chiloba amejiunga na orodha ya waliokuwa makamishna wa IEBC kuteuliwa kuhudumu nyadhifa mbalimbali serikalini, baada ya kujiuzulu.

Oktoba 2020, Rais Uhuru Kenyatta aliwateua Connie Maina, Paul Kurgat na Margaret Mwachanya kuhudumu nyadhifa za hadhi ya juu ubalozi wa Urusi, Italia na Pakistan, mtawalia.

Watatu hao walijiuzulu baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

You can share this post!

Azerbaijan yaitaka Armenia kukomesha kampuni zinazochafua...

WABUNGE waisuta TSC kwa kubebesha walimu mzigo wa mafunzo...