• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:50 AM
Vijana wa UDA Mlima Kenya watoa onyo kwa Maina Njenga 

Vijana wa UDA Mlima Kenya watoa onyo kwa Maina Njenga 

NA MWANGI MUIRURI 

MUUNGANO wa vijana wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) sasa unamtaka aliyekuwa kinara wa kundi haramu la Mungiki amulikwe kwa karibu na vitengo vya kiusalama.

Mwenyekiti wa muungano huo Bw Stephen Warui, akizungumza katika mji wa Kerugoya Julai 16, 2023, alidai kwamba kuna uwezekano kwamba kundi hilo haramu linarejea mashinani.

“Tangu siasa hizi za maandamano zianze kuvuma hapa nchini, tumeshuhudia baadhi ya vijana wenzetu wakiingia katika mtego wa kurejelea mienendo potovu ya itikadi za Mungiki,” akasema.

Bw Warui alisema kuwa kuna madalali wa kisiasa ambao wamekuwa wakizuru maeneo ya Mlima Kenya, wakisajili vijana ili washiriki maandamano.

“Upelelezi wetu umebaini kwamba vijana hao hupewa kati ya Sh500 na Sh3, 000 ili kushiriki maandamano hayo katika Kaunti za Mlima Kenya.

“Tuko na ushuhuda kwamba vijana wengi huagizwa washiriki maandamano hayo kama wafuasi wa Mungiki,” akasema.

Aliongeza kwamba “tunashuku kwamba Bw Njenga anahusika na njama hii akishirikiana na mwanasiasa mwingine aliyestaafu kutoka Ikulu hivi majuzi”.

Hata hivyo, Bw Njenga amekuwa akikana madai hayo akishikilia kwamba ni njama ya wanasiasa wa serikali ya kumharibia sifa na kunyanyasa vijana wanaoamka kila uchao kudai gharama ya maisha iteremshwe.

Bw Warui alidai kwamba “bora tu Bw Njenga, wafuasi wake na serikali, pamoja na upinzani kwa pamoja wakae wakijua tu hatutakubali kundi la Mungiki lirejee hapa nchini na kwa vyovyote vile tutasimama kidete kukataa”.

Mei 2023, Njenga alikamatwa na baadaye kuachiliwa na korti kwa dhamana kwa tuhuma za kuendeleza oparesheni kufufua kundi haramu la Mungiki.

Vuguvugu hilo lenye mizizi yake eneo la Mlima Kenya, limepigwa marufuku.

 

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Kamene Goro ashangazwa na matamshi ya mumewe DJ Bonez kuwa...

Vibarua wa kiume walalamikia mabroka wa bidhaa za mashamba...

T L