• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Vibarua wa kiume walalamikia mabroka wa bidhaa za mashamba kupendelea wanawake kimalipo  

Vibarua wa kiume walalamikia mabroka wa bidhaa za mashamba kupendelea wanawake kimalipo  

NA MWANGI MUIRURI
VIBARUA wa kiume katika udalali wa bidhaa za mashamba wametangaza kususia kazi kuanzia wiki ijayo wakiteta kwamba washirikishi wao wanapendelea wanawake.

Wakiongea na waandishi wa habari katika mji wa Makutano ulioko Kaunti ya Embu, walisema kwamba washirikishi hao wanasajili wanawake wengi kupita kiasi katika sekta hiyo na kisha kuwapa mishahara minono.

“Lori moja inafaa kuwa na vibarua saba ambao hushiriki kuvuna, kuchambua gredi na kisha upakiaji. Washirikishi wetu kwa vigezo ambavyo sio vya utendakazi wanasajili wanawake wanne na wanaume watatu,” akasema msemaji wa muungano wa vibarua wa udalali wa mavuno eneo la Makutano Bw Cyrus Mbithi.

Bw Mbithi alisema kwamba “kazi ya kuvuna na upakiaji huhitaji nguvu nyingi na wanawake hao hulemewa na kuishia kuwafanyisha wanaume walio katika ajira hiyo kazi ya punda”.

Lakini cha kugadhabisha zaidi ni kwamba, akaongeza, “wanaume hao wakilipwa Sh800 kwa siku, wanawake hao ambao walifanya kazi ndogo ikilinganishwa na wenzao wa kiume hulipwa Sh1 ,200 kila mmoja”.

Bw Mbiti alisema “Kuna zaidi ya malori 400 ambayo hufanya kazi hiyo ya udalali kwa niaba ya wafanyabiashara wa miji mikuu nchini…Malori hayo husaka bidhaa katika mashamba ya Kaunti za Embu, Machakos, Kirinyaga, Nyeri na Nyandarua”.

Alisema kuanzia wiki ijayo hakuna kibarua wa kiume ataabiri malori hayo “ili tuone jinsi wanawake hao na washirikishi wa udalali watawezana na kazi hiyo ngumu”.

Bw Mbiti alisema kwamba wamiliki wa malori hayo wanafaa wawaonye washirikishi wao wa udalali dhidi ya mapendeleo hayo ya kijinsia.

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Vijana wa UDA Mlima Kenya watoa onyo kwa Maina Njenga 

Wakulima Mlima Kenya wamtaka Gachagua awatimizie ahadi...

T L