• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Viongozi waisifu IEBC kwa kukaza kamba

Viongozi waisifu IEBC kwa kukaza kamba

NA LAWRENCE ONGARO

VIONGOZI kadha kutoka kaunti ya Kiambu wamepongeza juhudi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kukataa kuwaidhinisha wanasiasa walio na doa.

Viongozi hao walisema hatua hiyo inaongeza imani ya wananchi kwa tume hiyo inavyo endesha kazi yake kwa uwazi.

Wakiongozwa na mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Wajungle’ Wainaina, walisema iwapo tume hiyo itaendelea na mtindo huo wa kukabiliana na viongozi wafisadi, bila shaka “tutakuwa na viongozi wenye maadili mema.”

Alisema hata jamii ya kimataifa itakuwa na imani na tume hiyo huku viongozi watakaochaguliwa wakiwa ni wenye maadili mema.

Mbunge huyo alitoa wito kwa IEBC ionyeshe uwezo wake wa kufanya uchaguzi wa haki na uwazi bila kufuata matamshi yanayoelezwa na viongozi.

Askofu wa kanisa la Calvary mjini Thika Bw David Kariuki Ngari alitaka vitengo vinavyopambana na maswala ya ufisadi viendeshe kazi yao kwa uwazi na uwajibikaji bila maonevu yoyote.

“Tungetaka kuona yeyote anayepatikana na hatia ya ufisadi achukuliwe hatua za kisheria ili haki ionekane kutendeka,” alifafanua Askofu Ngari.

Alisema Rais Uhuru Kenyatta amejaribu kupambana na ufisadi licha ya vizingiti vilivyoko.

Alipendekeza kwamba rais atakayechaguliwa afanye juhudi kuendeleza miradi yote iliyozinduliwa na Rais Kenyatta.

Askofu Ngari ambaye anawania kiti cha ubunge Thika anasema yuko tayari kuwatumikia wakazi wa Thika bila ubaguzi wowote.

Bw Aloyce Kinyanjui, anayewania kiti cha Juja, alipongeza IEBC na kusema waendelee kukaza kamba kwa viongozi wasiofuata sheria za uchaguzi.

“Tunataka kuona viongozi waadilifu ndio wanapewa nafasi ya kuwania viti vya uongozi. Wafisadi wanastahili kuwekwa kando,” alifafanua Bw Kinyanjui.

Aliwarai wapigakura kuwachagua viongozi wenye rekodi safi ya uongozi.

Alisema wangetaka kuona wananchi wanachagua viongozi walio na rekodi safi walio na nia njema ya kuleta maendeleo kwa wananchi.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: IEBC izibe mianya ya kutilia shaka uchaguzi

TIBA NA TABIBU: Kulegea, kuoza kwa meno inaweza kuwa dalili...

T L