• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Waandamanaji wapeleka maiti kwa ofisi ya serikali

Waandamanaji wapeleka maiti kwa ofisi ya serikali

Na KALUME KAZUNGU

WAANDAMANAJI wenye ghadhabu kisiwani Lamu, Jumanne walizua kioja walipobeba maiti ya mwanamume aliyefariki akiwa na umri wa miaka 32 hadi kwenye ofisi ya Naibu Kamishna wa kaunti ya Lamu na kuacha maiti hiyo mlangoni.

Marehemu, Kalume Cheu, ambaye ni mfanyakazi wa kuchomelea vyuma, alikumbana na mauti yake pale alipovamiwa na genge la wanaume waliojihami kwa visu na mapanga na kumdunga upande wa tumbo na kumuua papo hapo kabla ya kutoweka na simu yake ya mkononi.

Bw Cheu ni mkazi wa kaunti jirani ya Kilifi na alikuwa akifanya kazi zake za vibarua Lamu.

Alikimbizwa hospitalini na marafiki pamoja na majirani zake baada ya uvamizi huo wa Jumatatu majira ya saa kumi na mbili jioni lakini akatangazwa kuwa amefariki punde alipofika hospitalini humo.

Tukio hilo lilizua ghadhabu miongoni mwa wakazi, wengi wao wakiwa ni wale wa kutoka kaunti nyingine wanaoishi Lamu, ambapo waliafikia kushiriki maandamano makubwa wakiwa wameubeba mwili wa mwendazake hadi kwenye ofisi hiyo ili kudai haki ya mpendwa wao.

Msemaji wa waandamanaji hao, Pascal Kashero alilaani vikali mauaji ya Bw Cheu na kuitaka idara ya usalama Kaunti ya Lamu kuwajibika na kuhakikisha waliohusika na mauaji hayo wanakamatwa na kushtakiwa.

“Tumeamua kuja kwa ofisi ya kamishna wa Lamu kudai haki kwa mwenzetu aliyeuawa. Tunahisi kulengwa bila hatia. Si mara ya kwanza mauaji kamahaya yanafanyika hapa kisiwani. Hatutaondoka hapa. Tutakaa nah ii maiti hadi pale walinda usalama watakapowaleta waliohusika na mauaji ili tuwafahamu.Tumechoka,” akasema Bw Kashero.

Lucy Kazungu alieleza masikitiko yake kwamba hakuna yeyote ambaye hadi sasa amehukumiwa kutokana na mauaji ya wenzao yaliyofanyika awali.

Bi Kazungu aliwakashifu polisi wa Lamu kwa uzembe katika kudhibiti usalama wa wananchi.

“Polisi wa hapa wameelekeza nguvu zao katika kuwakamata wasiovaa barakoa na kuwapora fedha zao lakini hawazingatii usalama wetu kama wananchi. Tutaendelea kushuhudia maafa ya mapanga na visu kwa watu wetu hadi lini? Polisi wawajibikie jukumu lao,” akasema Bi Kazungu.

Binamu ya mwendazake, David Ziro alimtaja marehemu kuwa mpenda amani na ambaye hakuwa na kisasi na yeyote.

“Yeye ni mpenda watu. Hapendi vita.Ninashangaa kwamba watu wanamvamia kakangu na kumuua. Naomba haki itendeke kwa Cheu,” akasema Bw Ziro.

Naibu Kamishna wa Lamu ya Kati, Philip Oloo na Afisa Mkuu wa Polisi wa eneo hilo, Geoffrey Osanane waliwaomba waandamanaji kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea kuhusiana na waliohusika na mauaji hayo.

“Ninawasihi muuchukue huu mwili hapa mlangoni kwangu mrudi nao mochari ili kupisha uchunguzi wetu uendelee. Hiki kitakuwa kisa cha mwisho cha mwananchi kupoteza uhai kwa kuvamiwa na wahalifu wenye visu na mapanga hapa kisiwani Lamu,” akasema Bw Oloo.

Bw Osanane alifichua kuwa tayari watu saba wanaohusiana na visa vya uvamizi kwa kutumia mapanga mjini Lamu tayari wamekamatwa na kufikishwa mahakamani na kwamba kesi zao zinaendelea.

Juhudi za maafisa hao kuwarai wananchi kuondoa maiti mlangoni ziligonga mwamba, hali iliyopelekea polisi kulipua vitoa machozi na kuwatawanya waandamanaji hao kabla ya mwili kuondolewa na kurudishwa hifadhi ya maiti ya hospitali ya King Fahad mjini Lamu.

  • Tags

You can share this post!

Bunge lasitisha shughuli Uganda kufuatia milipuko ya mabomu

Fainali za mashindano ya michezo ya vyuo vya kiufundi...

T L