• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:50 AM
Waasi ODM walilia Ruto awaokoe

Waasi ODM walilia Ruto awaokoe

Na GEORGE ODIWUOR

WABUNGE ‘waasi’ wa ODM wamelalamika kuwa baadhi ya wanachama wa chama chao wanawalenga kwa kuunga mkono serikali ya Rais William Ruto na kumtaka Kiongozi wa Nchi awaokoe.

Wabunge hao walisema wote wameitwa na kamati ya nidhamu ya ODM kueleza ni kwa nini walibadilisha uaminifu wao kutoka kwa kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga hadi kwa Rais Ruto.

Wabunge hao ni Caroli Omondi (Suba Kusini), Mark Nyamita (Uriri), Gideon Ochanda (Bondo), Elisha Odhiambo (Gem), Felix Odiwuor (Langata), Paul Abuor (Rongo) na Seneta wa Kisumu Tom Ojienda.

Bw Odiwuor alisema alipokea barua kutoka kwa chama chake akijulishwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu.

Kwa hivyo, aliomba usaidizi kutoka kwa Bw Ruto ambaye alimuunga mkono.

“Kosa langu kubwa lilikuwa kuunga Serikali. Rais Ruto kwa hivyo anafaa kuzungumza na Raila Odinga ili kuniokoa,” Bw Odiwuor alisema.

Wakizungumza mbele ya Rais Ruto alipozuru Kaunti ya Homa Bay, Jumamosi, wabunge hao walisema masaibu yao yanatokana na kushirikiana na serikali.

Wabunge hao wanatarajiwa kuhojiwa na kamati ya nidhamu ya ODM kuhusu sababu za kuunga mkono serikali ambayo Upinzani unaipiga vita.

Lakini pia watatumia fursa hiyo kujitetea na kuieleza kamati kwa nini wasichukuliwe hatua.

Baadhi ya viongozi wa ODM wanataka wabunge hao wafurushwe chamani na uchaguzi mpya uitishwe katika maeneo-bunge yao.

Imebainika kuwa baadhi ya wabunge hao wanahangaishwa na viongozi wakuu wa chama kwa uamuzi wa kisiasa walioufanya.

Bw Nyamita alisema wanashinikizwa kuacha kufanya kazi na serikali.

Lakini alijitetea kwa kuunga serikali na kusema kwamba hakuna ubaya kumtaka Rais kuwafanyia kazi watu wa Migori anakotoka.

“Tutaenda kujitetea. Lakini ninajua kwamba nilikuwa na dhamira nzuri ya kutafuta usaidizi kutoka kwa Serikali, ni kwa manufaa ya watu wetu,” Bw Nyamita alisema.

Mbunge huyo pia aliwatetea wenzake akisema kila wanapokutana na Rais hawajadili siasa bali wanajishughulisha na masuala ya maendeleo pekee.

Bw Omondi alisema pia alipata barua iliyomtaka aeleze ni kwa nini anamuunga mkono Dkt Ruto.Alijitetea akisema kushirikiana na serikali hakumaanishi kuwa alikihama chama chake na kujiunga na Kenya Kwanza.

Kulingana na mbunge huyo wa Suba Kusini, alikuwa akitafuta maendeleo tu.

“Ujasiri ni kitu bora zaidi. Tutapigana hadi tushinde,” alisema.

Bw Omondi aliapa kuendelea kufanya kazi na Serikali ili eneo-bunge la Suba Kusini lipate maendeleo.

Bw Ojienda alisema atatumia ujuzi wake wa kisheria kuwatetea wenzake katika kamati ya nidhamu ya ODM.

Seneta huyo alisema anaelewa sheria inasema nini na kwamba hajazuiliwa kufanya kazi na Dkt Ruto.

“Katiba inatupa uhuru wa kufanya kazi na yeyote tunayemtaka,” Seneta Ojienda alisema.

 

  • Tags

You can share this post!

Wafanyakazi pabaya kampuni za sukari zikifungwa

Wanaume wanaopenda pombe wanaandamwa na magonjwa 60

T L