• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Wafanyakazi pabaya kampuni za sukari zikifungwa

Wafanyakazi pabaya kampuni za sukari zikifungwa

Na VICTOR RABALLA

WAKULIMA na wafanyakazi wa kampuni za sukari maeneo ya Nyanza na magharibi ya Kenya wanakodolea macho hali ngumu ya maisha baada ya kusitishwa kwa uzalishaji sukari nchini kwa zaidi ya miezi minne.

Uamuzi huo uliotangazwa na Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) unalenga kutoa nafasi kwa miwa kukomaa mashambani.

Mamlaka hiyo imezipa kampuni za sukari muda wa hadi Novemba 30, 2023 kurejelea shughuli za uzalishaji bidhaa hiyo.

Uamuzi huo ulitangazwa katika mkutano wa mashauriano uliofanyika mjini Kisumu Alhamisi wiki jana.

Kampuni za West Kenya na Olepito zinazoendeshwa na familia ya bilionea Rai zimesitisha shughuli za uzalishaji sukari ilhali kampuni ya Butali Sugari Mills inatarajiwa kusitisha shughuli leo, Jumatatu.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Butali Sanjay Patel alisema watatumia muda wa usitishwaji shughuli kufanyia ukarabati mitambo ya kiwanda chake.

“Tunawapongeza wakulima wetu kwa kuendelea kushirikiana nasi. Tunatarajia kurejelea shughuli hivi karibuni,” akasema kwenye taarifa.

Hata hivyo, hatima ya wafanyakazi haijulikani kwani kampuni hiyo haikutoa mwelekeo kuhusu kazi zao.

Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya West Kenya Sohan Sharma, hata hivyo alisema kuwa watachunguza upya hali baada ya miezi miwili, kwa lengo la kurejelea kazi.

“Kwa hivyo, ninaandika barua kushauri kuwa tutasitisha shughuli zetu kiwandani kuanzia Julai 14, 2023 hadi Novemba 30, 2023,” akasema.

Isipokuwa wale wanaohudumu katika idara muhimu, wafanyakazi wengine wote wataruhusiwa kwenda likizoni hadi Julai 31, 2023.

“Kampuni itatumia muda huu kufanya mashauriano na kisha kutoa mwelekeo kwa wafanyakazi na wakulima,” Bw Sharma akaongeza.

Hata hivyo, alisema kampuni hiyo imejitolea kutenda haki kwa wafanyakazi katika kipindi hicho ikizingatiwa hatua hiyo ni ya muda tu.

“Vile vile, tunashauri kuwa hii hatua ni ya muda kwani kampuni inanuia kurejelea shughuli za kawaida baada ya muda uliotajwa kwenye taarifa hii. Hizi ni nyakati ngumu kwa kila mtu na kampuni. Kwa hivyo, naomba uungwaji mkono kutoka kwenu ili sote turejee tukiwa sawa,” Bw Sharma akasema.

Ukosefu wa miwa kwa kipindi kirefu tangu mwanzoni mwa mwaka huu, umechangia kampuni za sukari kung’ang’ania malighafi hii.

Hali hii imesababishwa baadhi ya kampuni hizo kusaga miwa isiyokomaa na inayozalisha sukari ya thamani ya chini.

“Mbali na kushusha thamani ya sukari, mwenendo wa kuvuna miwa kabla ya kukomaa unawanyima wakulima faida. Hii ni kwa sababu miwa isiyokomaa ina uzani wa chini,” akasema mshirikishi wa vuguvugu la Sugar Campaign for Change (Sucam) Michael Arum.

Ili kuzisaidia kampuni za sukari zisifilisike, Chama cha Wafanyakazi wa Mashamba wa Miwa (KUSPAW) kimeitaka serikali kutoa leseni kwa kampuni hizo ili ziweze kuagiza sukari kutoka nje.

“Serikali iruhusu kampuni za sukari kuagiza sehemu kubwa ya tani 185,000 za sukari zinazohitajika nchini hadi Novemba 30, mwaka huu,” alisihi Katibu Mkuu wa KUSPAW, Francis Wangara.

 

  • Tags

You can share this post!

Madereva wa malori waapa kuendelea kugoma kila wiki huku...

Waasi ODM walilia Ruto awaokoe

T L