• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Wabunge wakataa wasichana matineja wasipewe tembe za kuzuia mimba

Wabunge wakataa wasichana matineja wasipewe tembe za kuzuia mimba

NA MASHIRIKA

KAMPALA, UGANDA>>>

WABUNGE wa Uganda wamekataa pendekezo la serikali kuruhusu wasichana wenye umri wa miaka 15 kupata tembe za kupanga uzazi ili kupunguza viwango vya juu vya ujauzito.

Naibu Spika Thomas Tayebwa, alitaja wazo hilo kuwa la kishetani.

“Kuwaruhusu wasichana wa miaka 15 kutumia njia za kupanga uzazi kutachangia visa vya unajisi kuongezeka,” akasema Tayebwa.

Afisa mkuu wa wizara ya afya alisema unyanyapaa unaowazunguka vijana wanaotumia njia mbalimbali za kupanga uzazi unapaswa kukomeshwa.

Takriban robo ya wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 19 nchini Uganda wana ujauzito huku wengine wakiwa na watoto. Idadi hiyo iliongezeka wakati wa janga la corona hasa baada ya shule kufungwa kwa takriban miaka miwili.

Wakati wa mjadala bungeni, Jumanne, Mbunge Lucy Akello alisaili ikiwa serikali iliamua kupunguza miaka ya kuanza kutumia njia mbalimbali za kupanga uzazi kutoka miaka 18 hadi miaka 15 au la.

“Sikuwahi kutumia njia mbalimbali za kupanga uzazi nikiwa mdogo. Natumia njia ya asili, niliyopewa na Mungu.”

Naye Waziri wa Afya ya Msingi, Margaret Muhanga alisema pendekezo hilo halijaidhinishwa na serikali bali limetolewa na Dkt Charles Olaro.
Aliuliza kama ni bora mtoto apate mimba na kisha kufa wakati akijifungua.

Dkt Olaro alisema kwamba kupata habari za afya ya uzazi sio suala la kuchagua tu bali ni suala la haki za kimsingi.

“Ni muhimu tujenge mazingira ambapo vijana wanaweza kupata habari kuhusu afya ya uzazi na wakihitaji bila unyanyapaa, ubaguzi, au hukumu,” Dkt Olaro alinukuliwa akisema.

Hata hivyo, naibu spika alisema pendekezo hilo halifai kuona mwangaza.

Kundi la viongozi wa kidini pia wamepinga pendekezo hilo, wakisema vijana wanapaswa kujiepusha na ngono.

  • Tags

You can share this post!

Whozu akiri hana kwake, ndio maana anaishi kwa mpenziwe...

Mke anataka kuniacha sababu mimi ni mkulima

T L