• Nairobi
  • Last Updated December 8th, 2023 10:25 PM
Wahitimu 6,500 kutoka MKU washauriwa wawe wabunifu

Wahitimu 6,500 kutoka MKU washauriwa wawe wabunifu

Na LAWRENCE ONGARO

WAHITIMU wapatao 6,500 wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) wameambiwa wawe wabunifu kwenye sherehe ya mahafali hao iliyofanyika Ijumaa.

Imeendeshwa kwa njia ya mtandao kitovu cha hafla hiyo kikiwa ni uwanja wa Happy Valley, Landless mjini Thika.

Mgeni wa heshima kwenye hafla hiyo, Prof Waswa Balunywa alitoa changamoto kwa serikali kuzingatia mtaala wa elimu ufaao ili kila mmoja awe na nafasi yake katika masomo.

Alisema elimu ya juu huambatanishwa na watu werevu pekee lakini ni vyema hata wale wasio na kiwango cha juu cha elimu kupewa nafasi yao ili kuleta maendeleo ya kiustawi katika nchi.

“Serikali ina nafasi kubwa ya kuweka sawa kiwango cha elimu kitakachosaidia kila mmoja ambaye ana ujuzi tofauti. Elimu isiangaziwe kuwa ya watu wachache lakini kila mmoja sharti awe na nafasi yake masomani,” alifafanua Prof Balunywa.

Alisema bara la Afrika lina rasilimali ya kutosha na ikilindwa na kutumiwa jinsi ipasavyo, bila shaka kila mmoja atapata nafasi ya kujikimu.

Alisema “tumetekwa nyara na jinsi nchi za magharibi zinavyojiendeleza lakini hatujagundua utajiri ambao upo katika bara letu la Afrika.”

Naye chansela wa MKU Prof John Struthers alipongeza shirika la Danish Refugee Council (DRC), kwa ushirikiano na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Mafunzo na Utafiti – United Nations Institute for Training and Research (UNITRA), kuwafadhili wanafunzi 35 kutoka chuo hicho kwa mafunzo ya utafiti.

Wakati huo pia chuo cha MKU kimefanya ushirikiano wa karibu na shirika la Women Enterprise Fund (WEF), kupitia kwa ufadhili wa serikali.

Alieleza kuwa shirika hilo la wanawake linawapa wanawake hamasisho kuhusu maswala ya kibiashara ili waweze kujiendeleza.

Alisema wakati wa janga la Covid-19, chuo hicho kilikuwa na mikakati kadha ambapo kilizingatia upanzi wa miti, na pia kujumuika na walemavu kwa kuwapa misaada ya viti vya magurudumu.

Alijivunia kuchapisha kitabu kwa ushirikiano na wanachama watatu kutoka chuo hicho kiitwacho ‘Unemployment Intervention in Africa‘.

Dkt Jane Nyutu ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa chuo hicho alitaja Covid-19 kama tishio katika “mazingira tunamoishi”.

Alisema katika muda huo kumekuwa na matukio mengi ambayo yameshuhudiwa miongoni mwao yakiwa ni pamoja na msongo wa mawazo, familia kutengana, na watu kujiua miongoni mwa mambo mengine.

Pia aliwapongeza wanafunzi wawili wa chuo hicho ambao ni Christopher Mwanza Arunga kutoka Kaunti ya Kakamega ambaye alipokea tuzo ya Sh3.6 milioni kwa kuunda mtambo maalum wa kutengeneza chakula cha mifugo na Bi Silvia Wanjiku Kangéthe aliyepokea laki tisa kwa ubunifu wa kuunda chokoleti maalum.

“Nyinyi wanafunzi mnaofuzu leo ninawashauri muwe wabunifu ili muweze kujitetea wenyewe bila kutegemea kuajiriwa,” alitoa ushauri kwa mahafali hao.

You can share this post!

Wanafunzi wanaougua corona hawaonyeshi dalili – Kagwe

Uthiru Vision tumepania kushriki ligi kuu Kenya lakini...