• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Wakenya wazimiwa fursa ya kutesa katika ‘TikTok Live’ kutoka Lebanon

Wakenya wazimiwa fursa ya kutesa katika ‘TikTok Live’ kutoka Lebanon

NA CHARLES WASONGA

WAKENYA wengi wanaoenda Uarabuni kufanya kazi wapatapo muda wa kupumzika huingia TikTok Live kwa makeke lakini hilo halitatokea kwa wengi baada ya serikali kusema haina mkataba na serikali ya Lebanon kuwaruhusu kufanya kazi huko.

Serikali imezima mipango yoyote ya kuwapeleka Wakenya nchini Lebanon kuhudumu huko kama wafanyakazi wa kigeni.

Kwenye taarifa, Idara ya Huduma za Uhamiaji imesema hatua hiyo imekuchukuliwa kwa sababu Kenya haijatia saini mkataba wowote wa leba na taifa hilo la Uarabuni.

“Kwa sababu hiyo, hakuna uhakika kwamba haki na masilahi ya Wakenya yatadumishwa katika nchi hiyo ya Lebanon,” akasema Bw J.K Cheruiyot ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi.

“Kwa sababu zilizotajwa hapo juu, serikali imeamuru kwamba hakuna Mkenya ataruhusiwa kusafiri kuenda Lebanon kufanya kazi huko hadi wakati usiojulikana,” afisa huyo akaongeza kwenye taarifa ambayo nakala yake ilitumwa kwa Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Uhamiaji Evelyne Cheluget.

Mnamo Agosti 4, 2023, Waziri wa Leba Florence Bore alifichua kuwa jumla ya Wakenya 283 wamepoteza maisha yao katika nchi za Mashariki ya Kati ndani ya miaka mitatu.

Akijibu maswali bungeni, Bi Bore alisema kuwa Wakenya hao waliaga dunia wakifanya kazi katika mataifa ya Ghuba, haswa, Saudi Arabia, Qatar na Milki za Muungano wa Kiarabu (UAE).

Waziri huyo alisema wengi wa Wakenya hutumbukia kwenye matatizo katika nchi hizo wanakoenda kufanya kazi kwa kupelekwa na kampuni zisizosajiliwa rasmi na Wizara ya Leba.

“Hii ndio maana afisi zetu za ubalozi katika mataifa hayo huwa hazina maelezo kuhusu waajiri ambao Wakenya hao wanahudumia. Hali hii hutoa mwanya kwa wengine wao kuteswa bila maafisa wetu kuwa na habari,” Bi Bore akasema.

Kwa Wakenya wengi katika mataifa ya Uarabuni, jioni wamalizapo kazi hupenda sana kuingia kwenye majukwaa ya mtandaoni kama TikTok Live kuonyesha mbwembwe na makeke yao ili kusudi kujituliza baada ya mchana wenye utitiri wa shughuli.

  • Tags

You can share this post!

Mashamba ya wakazi yazamishwa na uvunaji mchanga Mto Nzoia

Jinsi mtoto wa kupanga aliyeangamiza mamake Nyeri...

T L