• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 1:09 PM
Mashamba ya wakazi yazamishwa na uvunaji mchanga Mto Nzoia

Mashamba ya wakazi yazamishwa na uvunaji mchanga Mto Nzoia

NA KASSIM ADINASI

MGOGORO wa kimazingira na kijamii katika maeneo ya nyanda za chini za Mto Nzoia katika eneo la Alego Magharibi unatokota kufuatia uvunaji wa mchanga kupindukia.

Jamii jirani zinanyoosheana kidole cha lawama wakazi wa Alego Magharibi wakilaumu wenzao wa Ugenya kwamba shughuli zao za uvunaji wa mchanga zimesababisha ekari nane za shamba kuzama ndani ya maji ya mto huo.

Uchunguzi wa Taifa Leo umeonyesha kweli mto huo umeanzisha mkondo mpya katika eneo hilo, hali inayofanya baadhi ya mashamba kuzingirwa na maji na ‘kisiwa’ kujitengeneza.

Bi Everlyne Akinyi, 35, kutoka kwa kijiji cha Rapenji anasimulia masaibu ambayo wakulima wamepitia tangu kujiunda kwa mkondo huo uliosababishwa na uvunaji wa mchanga.

“Shughuli za wavunaji wa mchanga zimetutatiza sana huku kwa sababu mashamba yetu yameanza kuzama na kisiwa hiki kinahatarisha maisha yetu,” akasema Bi Akinyi.

Anaongeza kusema, “Uvunaji wa mchanga unafaa kufanywa katikati mtoni na wala sio katika kingo na sungosungo zake. Shughuli zao zimesababisha udongo mwingi wa mashamba yetu kurambwa na kuzamia mtoni. Tutatoa wapi riziki yetu ya kila siku?”

Naye Bw George Ouma, mkazi pia, analaumu Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira Nchini (Nema) kwa kushindwa kuchukua hatua licha ya kufahamishwa zaidi ya mara moja.

“Binafsi nimefika kwa ofisi za Nema zaidi ya mara tatu kuwapa maafisa malalamiko ya uvunaji haramu wa mchanga lakini inahuzunisha kwamba hawajachukua hatua yoyote na wavunaji hao wanaendelea kufanya kazi hiyo bila uoga,” akalalama.

Hofu kuu ya Bw Ouma ni kwamba mvua ya  El-Nino ikija, maji yake ya mafuriko yatafagia mashamba ya wakulima hao na kuongeza kiwango cha uharibifu.

“Vyombo vya habari vimewanukuu maafisa wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa wakisema tujiandae kwa mvua ya El Nino. Sisi tunaotegemea kilimo basi hatima yetu itakuwa mbaya,” Bw Ouma akasema.

Sehemu ambayo kingo za Mto Nzoia zimerambwa na wavunaji wa mchanga na kusababisha mashamba ya wakazi wa Alego Magharibi kuanza kuzama. PICHA | KASSIM ADINASI

Mgogoro wa kijamii, wakazi wamesema, unafaa kutatuliwa upesi.

“Mbunge wa Ugenya David Ochieng na mwenzake wa Alego Usonga Samuel Atandi wanafaa kuzileta jamii hizi mbili pamoja ili kutatua mgogoro,” Bw Ouma akasema.

Bw Sylvester Odinga anasema awali shamba lake lilikuwa na rutuba ya kutosha na kero ya wavunaji wa mchanga haikuwepo.

Yeye ni mkulima wa sukumawiki, kabeji, vitunguu na mahindi.

“Siku za nyuma wanunuaji wa bidhaa walikuwa wakija kununua mboga katika eneo hili na sisi wanajamii tulikuwa tukipata pesa kutokana na kilimo,”akasema Bw Odinga.

Wakazi hao wanataka suala hilo litafutiwe suluhu mara moja.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Joto la atakayevalia viatu vya Raila lashamiri

Wakenya wazimiwa fursa ya kutesa katika ‘TikTok...

T L