• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Wakongwe 6,000 kutoka Thika wanufaika na misaada

Wakongwe 6,000 kutoka Thika wanufaika na misaada

NA LAWRENCE ONGARO

WAKONGWE zaidi ya 6,000 kutoka eneo la Thika walipokea misaada ili wajikimu kimaisha.

Waziri wa Leba na Maswala ya Kijamii, Bi Florence Bore, alisema kwa muda wa mwezi mmoja wataandikisha wakongwe nusu milioni katika mpango wa Jamii ili wapate usaidizi wa kila mwezi.

Alisema wataendelea kuwasaidia walemavu na mayatima popote walipo kote nchini.

Aliahidi kwamba wanawake wajane pia watapewa usaidizi na serikali kwa kuwafungulia biashara.

“Serikali itafanya juhudi kuona ya kwamba wanawake hao wanapewa usaidizi wa kifedha ili waendeshe biashara zao,” alisema waziri Bore.

Mbunge wa Thika Bi Alice Ng’ang’a alisema wakongwe wa umri wa miaka 70 walinufaika na chakula, magodoro, na blanketi.

Baadhi ya wazee waliojumuika katika Shule ya Msingi ya St Patrick’s mjini Thika, Agosti 25, 2023, ambapo walipokea msaada. PICHA | LAWRENCE ONGARO

“Shughuli hiyo itaendelea hadi mwisho wa mwezi Septemba. Tunataka ifikapo wakati huo, kila mkongwe awe amepokea msaada huo,” alisema mbunge huyo.

Alisema serikali iko makini kuona ya kwamba kila mwisho wa mwezi kila mkongwe anapokea Sh2,000 bila kuchelewa.

Alisema mpango huo wa kutoa misaada utajumuisha walemavu na mayatima.

Alisema atazuru kaunti nyingine nchini kuona ya kwamba wakongwe na walemavu wananufaika kupitia ufadhili wa serikali.

“Gharama ya maisha iko juu. Serikali haitakubali kuona wakongwe, walemavu na mayatima wakitaabika,” alisema mbunge huyo.

Aliyasema hayo katika Shule ya Msingi ya St Patrick’s mjini Thika ambapo zaidi ya wakongwe wapatao 6,000 walijumuika huko kupokea misaada hiyo.

Walinda usalama walikabiliwa na wakati mgumu kwa sababu watu wengi walionekana waking’ang’ania misaada hiyo iliyoletwa kwa malori manne.

Wengi walionufaika na misaada hiyo walirejea makwao wakiwa wanatabasamu.

Wahudumu wa bodaboda walipata biashara ya haraka ya kuwasafirisha wanufaika pamoja na mizigo yao.

  • Tags

You can share this post!

Seneti kujadili hoja ya kuhalalisha Kamati ya Kitaifa ya...

Mzozo wa Malisho: Wakazi wa Vitengeni, wafugaji washikana...

T L