• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Wakulima wa mahindi wamlilia Linturi mabroka wakiwavamia na bei duni

Wakulima wa mahindi wamlilia Linturi mabroka wakiwavamia na bei duni

NA EVANS JAOLA NA LABAAN SHABAAN

WAKULIMA wa mahindi wamelaumu serikali kwa kukosa kutangaza bei za mahindi huku msimu wa mavuno ukiendelea kushika kasi.

Na wakati gharama ya juu ya maisha inazidi kuwauma wakulima, mabroka wameona mwanya wa kuwapunja wakulima waliokosa mwelekeo mwafaka wa serikali kuhusu bei ya chini ya kuuza mazao ya mihindi.

Hii imewafanya wakulima kutuma shutuma zao kwa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi kwa chelewa chelewa za kutangaza bei.

Kuna kilio cha wakulima katika kimoja cha vitovu vya vyakula Kenya: Kaunti ya Trans Nzoia.

Uchunguzi wa Taifa Leo katika kaunti hiyo, umefichua bei ya mahindi imeshuka sana.

Gunia la kilo 90 limeshuka bei kutoka Sh4,200 hadi Sh3,000 na Sh3,800 kutegemea kiwango cha unyevu na vigezo vingine vya soko.

“Serikali itakuwa na magunia machache ya mahindi katika maghala ya Halmashauri ya Kitaifa ya Nafaka (NCPB) kwa sababu wakulima wengi wameuza mahindi kwa kukosa njia ya kuhifadhi,” mkulima mmoja alisema akitaja sababu ya hali ngumu ya maisha.

Mkulima mwingine, Fredrick Rono, alilaumu serikali akisema imekosa kumlinda mkulima.

“Kwa nini serikali imechukua muda mrefu kutangaza bei na wanajua msimu wa mavuno? Linturi hafai kubembeleza matapeli katika sekta ya mahindi,” alisema Rono.

Hata hivyo, awali serikali iliwapa onyo wakulima wasihadaiwe na madalali wanaonunua mahindi kwa Sh3,000.

Aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Kilimo Harsama Kello aliambia wakulima kuwa serikali imeshirikiana na kampuni saba za kununua mahindi ili kuweka bei ya Sh4,200 kwa gunia.

Bw Harsama sasa ni Katibu wa Idara ya Ustawi wa Kanda, Maeneo Kame na Nusu Kame.

Hii ni baada ya mageuzi yaliyofanyika katika baraza la mawaziri Oktoba 4, 2023.

Serikali iliahidi kuweka mikakati ya kuhifadhi mavuno ya magunia milioni 44 yasiharibiwe na mvua za El Nino zinazotarajiwa.

Eneo la Kaskazini ya Bonde la Ufa linatarajiwa kuzalisha magunia milioni 22 ambapo Trans Nzoia itatoa mavuno ya juu ya magunia milioni 7 na Uasin Gishu izalishe magunia milioni 6.

Kulingana na Waziri wa Kilimo wa Trans Nzoia Phanice Khatundi, wakulima waliouza mazao yao wamepata hasara kubwa kwa sababu ya mabroka.

  • Tags

You can share this post!

El Nino itachelewa lakini inakuja, msipuuze, Wakenya...

Kinyanjui ajinyanyua mwaka mmoja baada ya kulambishwa...

T L