• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
Wakurugenzi wapya wa KTDA hawajaanza kazi

Wakurugenzi wapya wa KTDA hawajaanza kazi

Na VITALIS KIMUTAI

WAKURUGENZI wapya wa Shirika la Ustawi wa Majanichai (KTDA) katika viwanda vilivyo kusini mwa Bonde la Ufa, hawajaanza kazi sababu ya vizingiti walivyowekewa na mameneja wa shirika hilo.

Mameneja wa viwanda (FUMs) na maafisa wakuu hawajakutana na wakurugenzi hao wapya kuwafahamisha masuala ya kifedha na shughuli za viwandani, wiki tatu baada ya uchaguzi kukamilika.

Inasemekana mameneja hao wamepewa maagizo makali kutoka kwa wakuu wa shirika hilo wasishirikiane na wakurugenzi wapya, hadi kesi iliyo kortini kuhusu uhalali wa uchaguzi huo itakapoamuliwa.

“Tunakabiliwa na hali ngumu sana kwa kuwa mwajiri (KTDA) hataki tushirikiane na wakurugenzi wapya huku serikali na wakulima kwa upande mwingine wakitushinikiza tushirikiane na kundi jipya,” alisema meneja wa kiwanda kimoja.

lli kuepuka lawama za mwajiri, mameneja wamesusia mikutano inayoitishwa na wakurugenzi hao wapya ambao wamepokelewa na maafisa wa vyeo vya chini huku mzozo kuhusu uhalali wa uchaguzi ukiendelea.

Inadaiwa wakurugenzi hao wanapanga kuwachukulia hatua mameneja huku mikutano kadhaa ikitayarishwa wiki hii kujadili suala hilo.

Kwa upande mwingine, wakurugenzi kutoka viwanda vyote 69 vya KTDA wamekuwa wakikutana kupitia video, ili kupanga hatua za kuchukua dhidi ya kuzuiwa kwao kutwaa usukani wa viwanda.

KTDA haikuwa imejibu maswali ambayo idara ya mawasiliano iliomba itumiwe kupitia barua pepe Jumatatu asubuhi.

Haya yanajiri huku wakulima wa mashamba madogo ya chai kutoka kusini mwa Bonde la Ufa wakiomba serikali ihakikishe mageuzi katika sekta hiyo yametekelezwa kikamilifu.

“Tunaomba serikali ihakikishe kuwa mageuzi katika sekta ya chai yametekelezwa kikamilifu ili kutuwezesha kupata mapato bora baada ya miaka mingi ya kupata hasara tupu,” akasema Bw Cheruiyot Baliach, mkulima wa majanichai katika eneobunge la Konoin, Kaunti ya Bomet.

Bw Baliach alisikitika kuwa licha ya chai kuletea taifa la Kenya pesa nyingi za kigeni, wakulima wa mashamba madogo wamebaki kuishi katika hali ya umaskini bila cha kujivunia kwa jasho lao.

Naye Bw Peter Koech, ambaye ni mkulima wa chai kutoka Belgut, alihimiza wakurugenzi wapya wa viwanda kuweka mikakati kabambe kuhakikisha chai ya Kenya inapata masoko mapya.

“Ni muhimu kwa wakurugenzi wapya kushirikiana na serikali kutafuta masoko mapya ya chai yetu ili wakulima wanufaike na kitega uchumi hiki,” akasema.

You can share this post!

Jaji Koome atwaa afisi muhimu akiahidi mageuzi

Raila alakiwa kishujaa tayari kwa Madaraka