• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Jaji Koome atwaa afisi muhimu akiahidi mageuzi

Jaji Koome atwaa afisi muhimu akiahidi mageuzi

Na RICHARD MUNGUTI

JAJI Mkuu mpya Martha Koome ameapa kuhakikisha uhuru wa idara ya mahakama unazingatiwa na kutekelezwa, huku akiomba idara zote tatu za serikali zishirikiane kuhudumia wananchi.

Akihutubu baada ya kukabidhiwa rasmi vifaa vya uongozi wa Idara ya Mahakama, Jaji Koome alisema hapafai kuwepo ushindani kati ya Mahakama, Bunge na Serikali ya Taifa.

Aliahidi kuwa uongozi wake kama Jaji Mkuu, utaangazia zaidi utumizi wa teknolojia katika utoaji haki kwa wananchi.

Kauli yake inatokana na hali iliyochangiwa na janga la Covid-19, ambapo kesi ziliwasilishwa kwa kuorodhesha mitandaoni. Kesi hizo pia zimekuwa zikiendeshwa kwa njia hiyo hiyo, kupitia Zoom au Google Meet.

Alipokezwa afisi hiyo na Naibu wa Jaji Mkuu, Philomena Mbete Mwilu, ambapo aliahidi kuhakikisha idara ya mahakama inatekeleza kazi yake kwa njia huru.

“Hakuna hata mtu au taasisi itakayoruhusiwa kuvuruga uhuru na utendakazi wa idara ya mahakama,” akasema Jaji Koome. Jaji Mwilu alikuwa kaimu Jaji Mkuu kwa siku 134, tangu alipostaafu aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga mwezi Januari mwaka huu.

Jana, Jaji Koome alikariri msimamo wake kwamba atatekeleza majukumu yake ya kutatua shida kubwa ya msongamano wa kesi.

Alipokuwa akihojiwa ili kujaza nafasi hiyo, Jaji Koome alikiri kuwa wakati huo kulikuwa na zaidi ya kesi milioni moja ambazo hazijakamilishwa na kutolewa uamuzi.

Kulingana naye, hakuna kesi inayopaswa kukaa miaka mitatu kortini kabla ya kuamuliwa. Mwongozo wa idara ya mahakama unasema kila kesi inatakiwa kusikizwa na kuamuliwa kwa haraka.

Suala jingine muhimu ni kukosekana haki kwa wananchi kutokana na umbali wa mahakama. Pendekezo kuu la idara ya mahakama ni kila eneobunge liwe na mahakama ya hakimu na kila kaunti iwe na mahakama kuu.

“Kila mahakama inahitaji kutambua kuwa kila mmoja anayewasilisha kesi kortini anahitaji kupata haki,” alisema Jaji Koome.

Jaji huyo mkuu mpya alisema kila mmoja katika idara ya mahakama anapaswa kutekeleza jukumu lake kwa njia ipasayo ndipo wanaowasilisha kesi mahakamani wawe na imani na idara ya mahakama.

Hafla ya jana iliyofanyika katika mahakama ya juu ilihudhuriwa na Jaji mkuu (mstaafu) David Maraga, mwanamke wa kwanza nchini kuwa hakimu na jaji, Jaji (mstaafu) Effie Owuor, Jaji (mstaafu) Joyce Aluoch, Jaji (mstaafu) Richard Kwach, Gavana wa Meru Kiraitu Murungi, Spika wa Seneti Ken Lusaka na washirika kutoka nchi za kigeni.

Pia Rais wa chama cha wanasheria nchini (LSK) Nelson Havi alihudhuria, licha ya kupinga uteuzi wake (Jaji Mkuu Koome).

Jaji Mwilu na Bw Maraga walimshauri kuwa kazi atakayoanza kuifanya iko na changamoto tele.

Bw Maraga alimshauri Jaji Koome kuwa jambo kuu ni kila mmoja nchini kujua katiba imeweka mipaka na “kila asasi yapasa kuizingatia.”

You can share this post!

Sossion asema mbinu ‘chafu’ za TSC kamwe hazitagawanya...

Wakurugenzi wapya wa KTDA hawajaanza kazi