• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Wanawake wazungu wanatupenda sababu tuna nyama ya ulimi, sio ndumba, Beach Boys wa Lamu wasisitiza

Wanawake wazungu wanatupenda sababu tuna nyama ya ulimi, sio ndumba, Beach Boys wa Lamu wasisitiza

NA KALUME KAZUNGU

NI nadra sana kumpata mtalii, iwe ni wa kike au wa kiume mwambao wa Pwani akizunguka hapa na pale na mja mwenyeji ambaye mavazi yake yanamsawiri kama wa hadhi ya juu.

Aghalabu mara nyingi utawapata watalii hao wakitembezwa ufuoni au kujiburudisha hotelini wakiwa pamoja na vijana au wazee ambao mavazi yao na mwonekano ni wa kawaida sana.

Sifa kuu ya wanaume wengi wanaotoa huduma za watalii kwenye fuo za Bahari Hindi Lamu na Pwani mara nyingi ni ile ya mtu wa kawaida ambaye huwa ‘hajapiga pamba’ kali sana wanavyosema vijana.

Utawapata baadhi ya ‘beach boys’ wakiwa wameweka mashungi ya nywele.

Wengine utawapata wamefuga rasta na wengine wakitembea miguu peku bila viatu.

Kuna wanaojifunga vikoi na kuvalia suruali zilizotobokatoboka, mashati mararuraru au yaliyochanikachanika ilhali wakiwa mguu chuma (nyayo tupu), ikizingatiwa kuwa vijana hawa wana hulka ya kutopenda kuvaa viatu.

Wengine utawapata wakikosa kuvalia shati au wengine wakivaa vesti pekee na kuacha kifua na mabega wazi ilmradi watalii wawaone.

Baadhi yao utawapata wakipendelea kunywa pombe na kuvuta sigara.

Lakini baadhi wamevuka mpaka kiasi kwamba wanatumia dawa za kulevya kama bangi, kokeni na heroni, wengi wakikiri kuwa ni kupitia kuchanganya malevya hayo, ambapo huwawezesha kuichapa kazi yao vyema.

Cha kushangaza ni kwamba watalii wengi, hasa wale wa kutoka mataifa ya ng’ambo tangu jadi wamekuwa wakiishia kuendea hao wanaume wanaoonekana kujiachilia, ambapo hujenga urafiki nao na kuwaamini kiasi kwamba wengine huishia kuolewa nao.

Kundi la watalii waliozuru kisiwani Lamu awali. PICHA | KALUME KAZUNGU

Hali hiyo imekuwa ikiwasukuma baadhi ya watu kudai kuwa hawa wanaume wanaotoa huduma za watalii ufuoni hawafanyi hivyo bure bure bali kuna uwezekano wao kutumia ndumba au uchawi kuroga wateja wao (watalii) ili wawapende au kuvutiwa, kupagawa na kuganda nao kama kigaga.

Ikumbukwe kuwa ndumba, uchawi au urogaji ni uganga wa kienyeji unaotumiwa kwa kuponyesha au kudhuru.

Uchawi pia unaweza kuelezwa kama ufundi wa kutumia dawa au vitabu maalumu vya uganga ili kuleta madhara kwa mwingine anayelengwa.

Taifa Jumapili ilizama kutaka kujua kiundani iwapo ni kweli hawa wanaume wa kutoa huduma za matembezi ya watalii ufukweni Lamu na mwambao wa Pwani kwa ujumla wanatumia juju ama ni dhana mbaya tu kuwahusu?

Mwenyekiti wa Muungano wa Vijana wa kutoa Huduma za Watalii Ufuoni, Kaunti ya Lamu, Abdallah Ziwa alikana kuwepo kwa visa vya vijana wake kutumia nguvu za giza kama uchawi kuvutia watalii.

Badala yake, Bw Ziwa alisema ili kufaulu kwenye kazi ya huduma za matembezi ya watalii ufuoni, yeyote aliyejitosa kwenye sekta hiyo lazima awe ‘sungura mjanja’.

Bw Ziwa,72, ndiye mhudumu mzee zaidi wa matembezi ya watalii ufuoni, akiwa ametekeleza kazi hiyo kwa karibu miaka 48 sasa.

Anasema sababu zinazowafanya watalii kuwaacha watu waliovalia vyema na kutorokea kwa wanaume wenye muonekano wa hadhi ya chini au waliojiachilia zinatokana na kwamba watalii hao wanajua fika kwamba ni watu wa aina hiyo ndio watakaowasaidia kukimu kila hitaji lililowafikisha Pwani ya Kenya, iwe ni Lamu, Malindi, Mombasa, au Diani huko Kwale na kwingineko.

Ingawa hivyo Bw Ziwa anasikitika kuwa kuna watalii wanaozuru Kenya, hasa mwambao wa Pwani, kwa nia mbaya ya kulangua au kutumia dawa za kulevya, kufanya umalaya au ngono ya watoto, kujiingiza kwa tabia za ushoga, kunywa pombe na kutekeleza maovu mengine.

“Punde ninapovalia nadhifu, kupiga pasi nguo zangu, kuvaa suti na viatu vilivyokoleza kiwi vizuri, mzungu ataniogopa na kudinda kunifuata. Anajua kabisa akinijia mimi hatapata lile atakalo, hasa iwapo linahusiana na maovu kama vile dawa za kulevya, pombe, mwanamke au mwanamume wa kufanya ngono au ushoga naye. Ndiyo sababu wakakimbilia hao ambao hadhi yao ni kama ya chini vile. Vijana hawa mara nyingi ni wawazi. Wazungu huwaamini kiurahisi, hivyo kuwatumia sana kufaulisha ajenda zao wakiwa likizoni,” akasema Bw Ziwa.

Bw Ziwa anashikilia kuwa iwapo mbinu ya kutumia uchawi kuroga watalii kuvutiwa na wanaowahudumia ufuoni ipo, basi kwa kaunti ya Lamu ni kwa uchache mno.

“Naweza sema juju kama ipo basi si hapa Lamu. Pengine wenzetu wa maeneo mengine ya Pwani wanatumia. Ninachokuhakikishia, hasa kulingana na tajiriba yangu ya miaka mingi kwenye sekta hii ni kwamba hapa Lamu ‘beach boys’ wanawanasa watalii kwa sababu ya kujua kusema nao,” akasema Bw Ziwa.

Akaongeza: “Ingawa hivyo, baadhi ya watalii wanataka watu wa aina hii kwa sababu wakiwatuma dawa za kulevya wanawaletea, wakitaka mwanamke au msichana yeyote wanapendelea kulala naye pia wanaletewa. Kuna wazungu wengine hata ni masenge wanaokuja kufanya ushoga. Wanatumia hawa vijana wa hadhi ya chini kuwatuma waletewe waume au wake wenzao kufanya ushoga au usagaji nao,” akasema Bw Ziwa.

Kwa upande wake, Mohamed Abubakar, ambaye amedumu kwenye kazi ya matembezi ya watalii ufuoni kwa miaka 37, anasema mhudumu kwenye sekta hiyo ya matembezi ya watalii ufuoni lazima awe mfahamu au mjuzi wa mambo kuhusu eneo analohudumia.

Bw Mohamed Abubakar, mmoja wa wahudumu wakongwe wa watalii Lamu akibebea mtalii mkoba kisiwani Lamu. Anasema ujuzi wa ufahamu wa Lamu, lugha na mila ya mtalii husika na nchi anayotoka ni muhimu kufaulisha kazi ya aina hiyo. PICHA | KALUME KAZUNGU

Anasema sababu zinazowafanya wazungu wengi kuwapenda wao ni jinsi walivyo wakweli na wakwasi wa historia na mambo yote yanayoihusu Lamu.

Bw Abubakar anasema ili kufaulu kwenye sekta ya matembezi ya watalii ufuoni, lazima mja awe stadi wa kuisoma na kuifahamu mila na desturi ya mteja wake mzungu.

“Hawa wazungu wapendeleacho sana ni wewe mhudumu kuwaelewa. Wengi wanatembelea sehemu zetu kutoka mataifa mbalimbali ambayo yako na mila na desturi tofautitofauti. Lazima ujue mzungu huyu anatoka wapi na mila yake kule ikoje. Ni lipi nisimfanyie na lipi anapenda nimtendee. Ukijua hayo na ukiambatanisha na ujuzi wako wa ufahamu wa historia ya Lamu basi,” akasema Bw Abubakar.

Naye Omar Ali, mhudumu mwingine wa ufuoni kwa karibu miaka 30 sasa, anasema kama mhudumu wa matembezi ya watalii ufuoni, lazima mja kujihami na takwimu kama vile idadi ya watu wapatikanao Lamu, idadi ya punda, Lamu ilianza lini, kwa nini Lamu ikatambuliwa na Unesco kama mji wa kale na wa kihistoria na kadhalika.

“Hayo yote ukimfahamisha mzungu unamyeyusha kabisa moyo na nafsi, hivyo kukupenda na kukuganda kila anapozuru Lamu au pwani kwa likizo zake,” akasema Bw Ali.

Kwa upande wake, Charo Hinzano, mhudumu wa watalii eneo la Maweni huko Malindi, Kaunti ya Kilifi anakiri kuwepo kwa baadhi ya wenzao wanaotumia ndumba kuwachanganya watalii.

Bw Hinzano aidha anasema kufanya hivyo si jambo jema kwani mara nyingi upendo unaotokana na juju huwa ni utumwa na wa muda tu.

“Kuna wenzetu, hasa wale ambao hutafuta wazungu kuoa au kuolewa lazima waende kwa waganga kupewa dawa ambayo mara nyingi huwekwa kinywani. Punde wanapowafungulia wazungu vinywa vyao kuongea nao wanawachanganya kwani maneno yao huvutia wateja hao na kujihisi wana pendo fulani lisilo la kawaida. Lakini mara nyingi mimi huambia wenzangu huo ni utumwa manake lazima urudi kwa mganga kwani dawa huwa inaisha nguvu. Punde dawa inapoisha, penzi huwa linakatika. Wengi wameishia kulia baada ya kutorokwa na wapenzi wao wazungu,” akasema Bw Hinzano.

Naye Obrahim Ekadeli ambaye pia ni mtembezi wa watalii ufuoni anasema wazungu wengi huzuru Kenya kutazama mila na desturi za jamii.

Bw Ekadeli anawashauri wenyeji, hasa vijana wanaotoa huduma za matembezi ya watalii na wageni kuhifadhi mila na tamaduni zao ili kuwavutia watalii badala ya kujiingiza kwenye masuala potovu, ikiwemo uchawi, dawa za kulevya, unywaji wa pombe na kadhalika.

“Mimi natoka kaunti ya Turkana na nimekuwa Malindi na sasa niko Lamu nikifanya hii kazi ya matembezi ya watalii ufuoni. Nikivaa shuka yangu ya Kiturkana na kushika bakora basi. Hawa watalii huvutiwa na mimi. Wanatembea nami kila mahali na hata kuniweka mlinzi wa malango yao kwenye sehemu zao wanakoishi. Najivunia mila yangu,” akasema Bw Ekadeli.

  • Tags

You can share this post!

Nyakati ngumu makundi mengi yakishindwa kulipa mikopo ya...

Mbunge Alice Ng’ang’a asema Thika Mjini isipogawanywa...

T L