• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Wapelelezi wapata simu ya mwanafunzi wa Tetu aliyeuawa kinyama

Wapelelezi wapata simu ya mwanafunzi wa Tetu aliyeuawa kinyama

NA MERCY MWENDE

WAPELELEZI mjini Nyeri wamepata simu ya mwanafunzi wa chuo cha kiufundi cha Tetu Technical and Vocational College aliyebakwa, akauawa na mwili wake kutupwa kando ya barabara Jumapili usiku.

Simu hiyo ilipatikana mita chache tu kutoka pahala ambapo mwili wa Peris Nyaguthii uligunduliwa na wachunaji wa majanichai waliokuwa wakielekea shambani mnamo Jumatatu asubuhi.

Marehemu alikuwa amefungiwa kwenye gunia na mwili wake kutupwa katika shamba la nyasi ya mifugo, takriban mita 800 kutoka nyumbani kwao kijijini Kamahuro, kaunti ndogo ya Tetu.

Kando na simu, polisi pia walipata barua iliyokuwa imeandikwa kwa hati ya mkono ikakunjwa. Wapelelezi wa kesi hiyo sasa wameiweka siri barua hiyo huku wakijetetea kuwa ufichuzi wa habari iliyoandikwa kwenye barua unaweza ukawekwa wazi tu wakishakamilisha upelelezi.

Akizungumza na Taifa LeoKamanda wa Polisi wa kaunti ndogo ya Tetu Richard Masila, alisema kuwa simu ya mwendazake ilionekana kwanza mnamo Jumanne na wanafunzi wa shule ya umma waliokuwa wakielekea shuleni.

“Ilikuwa alfajiri, wanafunzi walipoiona simu hiyo barabarani ingawa waliamua kuipuuza. Lakini walipoiona tena jioni, waliamua kuwajulisha wazazi wao,” akaeleza Bw Masila.

Kwa sababu wazazi hao walikuwa tayari wamefahamishwa kuhusu uchunguzi unaondelea wa mauaji, walimjulisha mzee wa kijiji ambaye aliwasiliana na polisi.

“Mzee wa kijiji alichukua hatua za haraka kwa kulinda pahala hapo na kuhakikisha kuwa hapakusumbuliwa au kuvutia macho ya umma hadi polisi walipofika,” akasema mmoja wa wenyeji.

Wapelelezi pia waliwazuia watu waliokuwepo wasisome maandishi yaliyoandikwa kwenye barua.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa kaunti ndogo ya Tetu, maafisa wa upelelezi sasa wanachunguza maandishi yaliyoandikwa kwenye barua hiyo pamoja na mazungumzo ya mwisho ya simu ili kubaini marehemu aliwasiliana na nani kabla ya kifo chake.

Kabla ya kifo chake, marehemu alishinda na mamake Jumapili wakiwa Kanisani ingawa walitengana baada ya ibada.

“Aliniambia kuwa ndugu yake alikuwa amemtuma marashi ambayo hakuweza kuyapata katika soko letu hapa nyumbani,” akaeleza mamake marehemu Bi Anne Mwangi.

Hivyo, akaamua kwenda kuyanunua marashi hayo katika soko kubwa la Gateri, lililoko umbali wa kilomita tatu kutoka nyumbani kwao.

Lakini marehemu hakurudi nyumbani jioni hiyo na simu yake ilikuwa imezima. Mwili wake ulipatikana siku iliyofuata.

  • Tags

You can share this post!

Kijana aliyeachia masomo Darasa la Tatu atengeneza...

Polo ahepa demu aliyetaka ‘mpini’ siku ya kwanza

T L