• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Watahiniwa 2 wafukuzwa kwa kuongea Kijaluo

Watahiniwa 2 wafukuzwa kwa kuongea Kijaluo

NA GEORGE ODIWUOR

KWENYE tukio la kushangaza, shule moja katika Kaunti ya Homa Bay jana iliwatimua wanafunzi wawili ambao ni watahiniwa wa mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) kwa kuongea kwa lugha ya mama na uchochezi.

Mwanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari ya Lala alitimuliwa kwa kuongea kwa lugha ya mama. Mwenzake wa kiume akidaiwa kuwachochea wenzake darasani baada ya kusoma barua ya kumtimua mwenzake hadharani.

Wanafunzi hao wawili sasa watakuwa nyumbani kwa wiki mbili huku wazazi wao wakieleza wasiwasi kuwa hatua hiyo itavuruga maandalizi yao ya KCSE. Mwanafunzi wa kike alitimuliwa mnamo Septemba 28 baada ya kuzungumza kwa Kiluo wakati ambapo afisa kutoka Wizara ya Elimu alikuwa shuleni humo.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu, Bw Kennedy Nyamolo, mwanafunzi huyo alikiuka sera ya shule ambayo inaamrisha kuwa lugha inayozungumziwa na wanafunzi lazima iwe rasmi.

“Tuna sera kuhusu lugha. Hata hivyo, mwanafunzi huyo alikiuka sheria hii kwa kuzungumza kwa Kiluo mbele ya mgeni,” akasema.

Inadaiwa mwanafunzi huyo alikataa kuzungumzia suala hilo wala kukubali kuwa alikiuka sheria za shule. Bw Nyamolo alisema kuwa mwanafunzi huyo alikingwa na wenzake ambao mwanzoni hawakuwa tayari kutaja hadharani kuwa ndiye alizungumza Kiluo.

Baada ya kubainika kuwa ndiye alizungumza lugha ya mama, alitumwa nyumbani na akaagizwa kuwa arejee shuleni siku ya mwisho ya maandalizi ya KCSE.

Mwanafunzi wa kiume naye alitumwa kwa kuwachochea wanafunzi ambao walikuwa wakipinga kutimuliwa kwa mwenzao.

Alishtumiwa kwa kusoma hadharani barua ambayo Mwalimu Mkuu alimwaandikia msichana huyo kama njia ya kuwachochea wanafunzi wazue vurugu.

Mamake mwanafunzi wa kike , Bi Eunice Achieng’, alisema kuwa mwanawe huenda akafeli kupata gredi nzuri ya kumwezesha kujiunga na chuo kikuu.

Bi Achieng’ alisema kuwa mwanawe anapania sana kurejea shuleni ili aendelee na masomo yake.

“Masomo kwa sasa ni muhimu na wakati huu ndipo walimu wanawaandaa wanafunzi kwa mtihani. Mwanangu amekuwa akilia kuwa anapoteza wakati ilhali wenzake wanaendelea na masomo yao,” akasema Bi Achieng’. Mwanafunzi huyo alisema kuwa alifukuzwa kutokana na deni la karo ambalo ni Sh25,000.

“Naamini kuwa kufukuzwa kwake kulitokana na deni hilo na suala la kuzungumza Kiluo linatumiwa tu kama kijisababu,” akasema Bi Achieng’.

Usimamizi wa shule nao umesema kuwa umeagiza wazazi wa watoto hao wafike mbele ya bodi ya shule mnamo Oktoba 17. Bw Nyamolo alisema ni wakati huo ndipo kilio chao kitasikizwa.

Mkurugenzi wa Elimu Homa Bay, Bi Eunice Khaemba, alisema suala hilo ni dogo na akawataka maafisa wa elimu wa kaunti ndogo walichunguze.

  • Tags

You can share this post!

Wakili ‘feki’ aliyeshinda kesi 26 apata...

DOMOKAYA: Lejendari Kipchoge hakika hajaonyesha picha nzuri...

T L