• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 AM
Wakili ‘feki’ aliyeshinda kesi 26 apata uungwaji kutoka kwa Sonko, Atwoli

Wakili ‘feki’ aliyeshinda kesi 26 apata uungwaji kutoka kwa Sonko, Atwoli

NA MERCY KOSKEI

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko ameelezea nia yake ya kumsaidia mwanamume aliyekamatwa kwa madai ya kujifanya wakili wa Mahakama Kuu.

Kupitia mtandao wake wa Twitter Octoba 13, 2023, Sonko alifichua kuwa atamfadhili mwanamume huyo kwa jina Brian Mwenda kuendelea na masomo ya uanasheria katika Chuo cha Kisheria cha Kenya.

Sonko alishangazwa jinsi mwanamume huyo ambaye anadaiwa kuwa hajasomea sheria angeweza kutetea kesi 26 mahakamani bila kujulikana.

“Nitamsaidia na kumfadhili kwenda Chuo cha Kisheria ikiwa atakosa pesa. Mwanamume huyu amekuwa akijifanya wakili. Hakuwahi kuenda shule yoyote ya sheria.

“Mafanikio: Kesi 26 ziliwasilishwa mbele ya Mahakimu, Majaji wa Mahakama Kuu na Majaji wa Mahakama ya Rufaa na kushinda kesi zote 26, hadi alipokamatwa Alhamisi,” Sonko alisema.

Hata hivyo, Chama cha Wanasheria nchini (LSK) hapo hawali kilitahadharisha umma dhidi ya mwanamume huyo anayedaiwa kujifanya wakili na kuwalaghai wateja wasiojua.

Tawi la LSK Nairobi lilitoa taarifa Alhamisi, Oktoba 12, 2023, na kusema kwamba Mwenda si wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya, wala mwanachama wao.

 “Tawi lingependa kujulisha umma kwamba Brian Mwenda Njagi si Wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya, wala mwanachama wa Tawi,” walitoa taarifa kupitia mtandao wa Twitter.

LSK pia ilihimiza yeyote ambaye ana habari kuhusu Mwenda au mtu mwingine yeyote anayejifanya wakili kuripoti kwa mamlaka husika ili kuchukuliwa hatua.

“Wanachama wanahimizwa kutoa habari kuhusu mtu yeyote anayejifanya Wakili hili hatua inayofaa kuchukuliwa,” taarifa hiyo iliongeza.

Hata hivyo, Mwenda ameendelea kupata uungwaji huku wa hivi punde zaidi akiwa Katibu mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini, COTU, Fransis Atwoli  aliyesema uchunguzi wa haki na uwazi ufanywe ili kupima ujuzi na uwezo wake katika taaluma ya sheria.

Katika taarifa Octoba 13, 2023, COTU ilisema kuwa inasimama na Bw Mwendwa kwani kesi hiyo inaibua maswali muhimu kuhusu upatikanaji na ushirikishwaji wa taaluma nchini kenya.

“COTU inatoa wito kwa serikali ya Kenya kuchukua fursa hii kutambua utambuzi wa mafunzo ya awali nchini Kenya. RPL ni utaratibu uliothibitishwa kutambua njia mbalimbali za kujifunza na kutumia vipaji ambavyo havijatumiwa na vinaweza kulipeleka taifa letu mbele,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Sarakasi za maisha ya kimapenzi ya Nairofey na Yeforian...

Watahiniwa 2 wafukuzwa kwa kuongea Kijaluo

T L