• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Watano wakamatwa polisi wakitwaa vifaa vya kielektroniki

Watano wakamatwa polisi wakitwaa vifaa vya kielektroniki

NA SAMMY KIMATU

WAKAZI katika mitaa ya mabanda ya Mukuru iliyoko katika tarafa ya South ‘B’, kaunti ndogo ya Starehe wanaweza kulala kwa amani baada ya polisi kukamata washukiwa watano wanaodaiwa kuwa sehemu ya genge hatari inayojiita ‘Gaza’.

Mwishoni mwa wiki, makachero kutoka kituo cha polisi cha Industrial Area walifanikiwa kukamata washukiwa watano katika operesheni ambayo wenyeji walisema haijawahi kushuhudiwa.

Miongoni mwao walikuwa vijana wanne na mwanamke mmoja ambaye polisi walisema hutumia nyumba yake kuweka mali iliyoibwa kisha atafute soko.

Kamanda wa polisi eneo la Makadara, Bi Judith Nyongesa alisema washukiwa hao walikamatwa katika maficho yao katika eneo la Bundalangi, mtaani wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba.

Kamanda wa polisi eneo la Makadara, Bi Judith Nyongesa. PICHA | SAMMY KIMATU

Akiongea na Taifa Leo baada ya tukio hilo, Bi Nyongesa aliongeza kwamba washukiwa walipatikana na silaha mseto yakiwemo mapanga na visu.

“Japo vijana hawa wanaonekana kuwa wadogo kiumri, ni hatari zaidi kwa wa uhalifu kuvunja nyumba na kupora watu njiani wakiwatisha kwa panga na visu,” Bi Nyongesa akasema.

Kando ya silaha, alisema maafisa wake walifanikiwa kupata Kamera, tarakilishi, vifaa vya saluni na simu kadhaa zinazoaminiwa kuibwa kwenye operesheni yao.

Bi Nyongesa alisema wakazi katika mtaa wa mabanda wa Kayaba, Hazina na Maasai Village walilalamikia kuhangaishwa na genge hilo kwa muda mrefu.

Mdokezi wetu aliamabia Taifa Leo kwamba genge hilo hushirikiana na wenzao kutoka mtaa wa Mukuru- Kwa Reuben kubadilishana wakati wanatekeleza uhalifu.

Alisema alitumia kikosi chake spesheli almaarufu SPIV kukabiliana na wahalifu sugu.

Baada ya kukamatwa, washukiwa waliambatana na maafisa hao kutoka Budalangi huku wakazi wakishabikia tukio hilo na kuwasifu polisi kwa kufanya kazi nzuri.

“Kuanzia leo, tutapata angalau usingizi kwa sababu huwa hatulali tuhifofia kushambuliwa,” mhudumu wa M-Pesa eneo la Cluster ‘A’ Crescent, mtaani Kayaba akasema.

Isitoshe, washukiwa walipeleka hadi mtaa wa mabanda wa Maasai ambako kuna mshukiwa mwenzao baada ya kukiri wanakotumia kama maficho yao.

Miongoni mwa bidhaa zilizopatikana Kamera aina ya Canon EOS na Tarakilishi zilikuwa ni mali ya Shirika moja la Kikatoliki la Mukuru Promotion Centre (MPC) linalofadhili elimu na huduma za afya ya wakazi mitaani ya Mukuru.

Mukurugenzi wa MPC, Mtawa Mary Kileen aliwashukuru maafisa wa polisi na kuwapongeza kwa kazi nzuri.

“MPC ilipatia kijana wetu wa Kayaba, Bw David Safari Kamera na Tarakilisi wakati anapokuwa akisomea uanahabari kwa lengo la kukuza taaluma yake,” Mtawa Mary akasema.

Bi Nyongesa alisema tarakilishi ya MPC ilipatikana na maafisa wake katika mtaa wa mabanda Mukuru-Kwa Njenga, eno buge la Embakasi Kusini.

Duru za polisi zilisema washukiwa wanahusishwa na visa vingine vya uhalifu wakati wa Maandamano ya Azimio.

Kadhalika, uchunguzi wa polisi ulionyesha kwamba miongoni mwa walioamatwa kuna mshukiwa mmoja ana rekodi ya kukamatwa na kuhukumiwa kifungo mara kadhaa.

Vilevile, Bi Nyongesa amewaomba wananchi kushirikiana na polisi kutoa taarifa akisema ni wajibu wake kuongoza maafisa wake kuhudumia wananchi.

“Wananchi ni wateja au makastoma wangu ikifika ni wakati wa kuchapa kazi,” Bi Nyongesa asema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Azimio sasa wakubali mazungumzo na Serikali

Wazee wa Mlima Kenya wampongeza Uhuru Kenyatta kwa...

T L