• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Watoto wa aliyekuwa mwenyekiti wa ‘Men’s Conference’ wapeleka mzozo kortini

Watoto wa aliyekuwa mwenyekiti wa ‘Men’s Conference’ wapeleka mzozo kortini

NA TITUS OMINDE

MZOZO wa urithi wa mali ya mabilioni ya aliyekuwa mwanasiasa na mfanyabiashara marehemu Jackson Kibor, umefikishwa mahakamani huku watoto wake 27 wakitaka kuhakikiwa kwa wosia ambao wameupinga wakiuita feki.

Hatua hiyo inajiri huku watoto wa wajane wawili wakionekana kushirikiana dhidi ya mjane mdogo wa marehemu Bw Kibor wakidai kuwa uhalali wa wosia huo unatiliwa shaka.

Kwa pamoja walidai kuwa wosia huo ni feki na hauakisi matakwa ya marehemu baba yao.

Kufuatia ombi hilo ambapo watoto 27 wanapinga wosia husika, Mahakama Kuu mjini Eldoret inafanya kikao leo Jumatano pamoja wahusika kwenye kesi hiyo ya urithi ili kuanzisha utaratibu wa kisheria kuharakisha kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi hiyo.

Mnamo Jumatatu Jaji Reuben Nyakundi aliagiza wahusika wote katika kesi hiyo wawepo mahakamani wakati wa mjadala kuhusu hali ya kesi hiyo.

“Mahakama inakusudia kuweka siku tatu za kusikilizwa kwa kesi hii ili kuharakisha usikilizwaji na uamuzi wa mzozo husika unakamilishwa kwa haraka. Tusipoteze mwelekeo wa kesi ili haki ipatikane katika suala hili,” alisema Jaji Nyakundi.

Familia ya marehemu imezama katika vita kuhusu usimamizi na ugavi wa mali ya marehemu Kibor inayokadiriwa kuwa zaidi ya Sh16 bilioni na kuenea Uasin Gishu, Trans-Nzoia, Nakuru, Nairobi na Mombasa.

Mzee Kibor alifariki akiwa katika hospitali ya Eldoret mapema 2022 baada ya kuugua kwa muda mrefu. Aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80.

Mali hiyo iliyoko kwenye mzozo ni pamoja na maelfu ya ekari za ardhi ya kilimo katika eneo la North Rift, majengo ya biashara katika miji mikuu ya Eldoret, Nairobi, Nakuru, amana za benki miongoni mwa nyingine.

Watoto 27 wa wajane wawili wa marehemu wamekana wosia ambao mke wa nne wa marehemu, Eunita Kibor, anadai kuwa ni hati ya kweli ambayo tajiri huyo aliiacha kama mwongozo na matakwa yake kuhusu namna utajiri wake unapaswa kugawanywa.

  • Tags

You can share this post!

Sasa ni rahisi Wakenya kupata huduma za serikali kidijitali...

Kizaazaa wazazi, wanafunzi wakiidai kaunti pesa zao

T L