• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Watoto wapewe basari bila ubaguzi – Magoha

Watoto wapewe basari bila ubaguzi – Magoha

Na WACHIRA MWANGI

WAZIRI wa Elimu, Prof George Magoha, ametaka ufadhili wa karo kwa watoto wa shule uwe ukitolewa kwa njia wazi bila ubaguzi wowote.

Akizungumza jana alipotembelea baadhi ya watoto ambao watapokea ufadhili kutoka kwa mpango wa Elimu Scholarship Awards mtaa wa Bangladesh, Mombasa, Prof Magoha alisema wizara yake imepanga kuongeza idadi ya watoto watakaokuwa wakinufaika na ufadhili huo.

“Ninafuata agizo la Rais Uhuru Kenyatta ili kuhakikisha baadhi ya watoto wanaofadhiliwa ni wa kutoka mitaa ya mabanda. Ufadhili huu unafaa kuwasaidia watoto kama hawa,” akasema.Kulingana naye, mpango huo unalenga kuwafikia watoto 9,000 kitaifa lakini amepanga kumshawishi Rais kwamba idadi iongezwe hadi 18,000.

Ufadhili huo hutolewa na serikali kupitia kwa Wizara ya Elimu kwa ushirikiano na Benki ya Dunia na Benki ya Equity.Prof Magoha alisifu Wakfu wa Benki ya Equity kwa jinsi wakfu huo ulivyochagua watoto wenye mahitaji na kusambaza ufadhili.

Mpango huo mwaka huu umelenga kaunti ndogo 110 katika miji 15 ambayo ni Thika, Garissa, Nairobi, Machakos, Eldoret, Kitui, Nakuru, Kericho, Mombasa, Kilifi, Kisumu, Naivasha, Nyeri, Kakamega na Embu.

Watoto wanaoishi katika mitaa ya mabanda na wale walio na mahitaji waliosoma katika shule za umma na kupata alama 280 kuenda juu katika Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) wanalengwa.

  • Tags

You can share this post!

Kesi ya Echesa kusikizwa faraghani

Pesa za wazee ziwafae wajane