• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Watoto zaidi ya 2,000 waambukizwa HIV kwa kunyonyeshwa

Watoto zaidi ya 2,000 waambukizwa HIV kwa kunyonyeshwa

Na MAUREEN ONGALA

WATOTO 2,331 wanaoishi Kaunti ya Kilifi waliambukizwa virusi vya HIV katika kipindi cha janga la corona kilichoanza nchini mwaka uliopita, serikali ya kaunti hiyo imesema.

Waziri wa Afya katika Kaunti ya Kilifi, Bw Charles Dadu jana alisema kuwa, kati ya idadi hiyo watoto 506 ni wa kiume na 1,825 wa kike.

Kulingana na Bw Dadu, waliambukizwa virusi hivyo kwa kunyonyeshwa na mama zao.Janga la corona lilipozuka nchini, wataalam wa masuala ya afya pia waliibua hofu ya watu kuogopa kufika hospitalini kwa matibabu ya maradhi mengine.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), mama aliyeambukizwa ukimwi anaweza kuzuia kuambukiza mtoto kwa kutumia dawa zinazopunguza makali ya virusi hivyo za ARV.

Lakini imebainika ni watoto 903 pekee kati ya walioambukizwa HIV Kilifi wakati huo ndio wako katika mpango wa kupokea dawa hizo za ARV.

Jumla ya kina mama 6,972 pia wanapokea dawa hizo.Watoto ambao waliandikishwa kupokea dawa za ARVs, wamewekwa pia kwenye mpango maalum unaoshirikisha serikali ya Kaunti na shirika la Amerika la kutoa misaada (USAID).

Vile vile, serikali ya kaunti imeshirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya watoto (UNICEF) kuendeleza mpango wa kuwapa watoto hao lishe bora. Watoto hao watapokea pesa kila mwezi ambazo wazazi wao wanatarajiwa kutumia kugharamia chakula.

You can share this post!

Wazazi watozwa ng’ombe 100 kwa utundu wa watoto wao

Kilio Taveta usimamizi wa shamba la Ruto ukikausha Ziwa Jipe