• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Kilio Taveta usimamizi wa shamba la Ruto ukikausha Ziwa Jipe

Kilio Taveta usimamizi wa shamba la Ruto ukikausha Ziwa Jipe

Na LUCY MKANYIKA

WAKULIMA katika eneo la Taveta, Kaunti ya Taifa Taveta, wamelalamikia athari ambazo zimeanza kuonekana kutokana na shughuli za shamba kubwa eneo hilo la ekari 1,000 linalomilikiwa na Naibu Rais Dkt Willliam Ruto.

Wakulima hao pamoja na wavuvi wamedai kuwa wasimamizi wa Kisima Farm wamezuia mradi wa kuzibua kijito cha Sombasomba, na hivyo kusababisha kupungua kwa viwango vya maji katika Ziwa Jipe.

Ziwa hilo hutegemewa na zaidi ya watu 3,000 kwa shughuli za uvuvi, ukulima na unyweshaji mifugo maji.Zamani shamba hilo lilikuwa linamilikiwa na aliyekuwa mbunge wa Taveta, Basil Criticos.

Utafiti uliofanywa na wanasayansi kutoka kwa Taasisi ya Utafiti wa Maswala ya Bahari na Samaki (Kemfri) mwaka jana, ulibainisha kuwa idadi ya samaki ziwani hilo imepungua sawa na viwango vya maji.

Mnamo Jumatano, maafisa kutoka mamlaka ya kusimamia rasilimali za maji nchini (Warma) walilazimika kufanya kikao na wakulima, wavuvi, viongozi na wasimamizi wa shamba hilo katika ukumbi wa Kimala ili kujaribu kutatua mzozo huo.

Meneja wa shamba hilo, Bw Aries Dempers aliyehudhuria mkutano huo, alilaumiwa kwa athari zinazokumba Ziwa Jipe.Naibu chifu wa Kachero, Bw Sharia Bwire alisema kuwa wenyeji wanakosa maji ya kunyunyiza mashambani na vilevile ya kunywesha mifugo wao.

“Alipoziba kijito nilituma mzee wa mtaa kumwambia mwekezaji aache maji yapite, lakini alikataa na kumwambia kuwa alitaka amri ya mahakama ili afanye hivyo,’ akasema Bw Bwire.

Bw Lawrent Kipesha, mmoja wa wakulima waliohudhuria kikao hicho, alisema kuwa wanakadiria hasara kubwa baada ya mimea yao kusombwa na maji wakati wa mvua kwani maji ya mvua yamezibiwa njia kuelekea ziwani.

‘Tangu 2019 sijaweza kufanya ukulima shambani kwangu kwa sababu ya mafuriko. Nilikuwa na miti ya minazi, migomba ya ndizi na matunda mengine lakini yote yalisombwa na maji. Wengi wanajua nilikuwa mkulima mashuhuri katika eneo hili lakini nimeacha ukulima kwa sababu ya mafuriko,’ akasema.

Diwani wa wadi ya Mata, Bw Chanzu Kamadi alisema mradi wa kuzibua mto umekwama kwa kuwa wasimamizi wa Kisima Farm walikataa kufungua ua wa shamba lao ili kuruhusu shughuli hiyo kuendelea.

‘Tumejaribu mara nyingi sana kumuomba meneja afungue ua huo lakini amekuwa akikataa,’ akasema.Katika mkutano huo, Bw Dempers alisema yuko tayari kufungua ua huo lakini akaomba ajulishwe mipangilio na wale watakaokuwa wakitekekeza mradi huo ili wajuane.

Mwaka uliopita, Bw Dempers alituhumiwa kwa kufunga bomba la maji ya kunywa lililokuwa likisambaza maji kwa wenyeji wa Jipe. Vilevile, alizuia maafisa wa maji wa Kaunti ya Taita Taveta kuingia shambani humo kukagua bomba hilo.

Mwaka juzi, meneja huyo vilevile alikamatwa na polisi baada ya kuvamia msikiti mmoja wa Jipe na kuwatishia kwa bastola waumini waliokuwa wakitekeleza ibada yao ya alfajiri.

Bw Dempers vilevile alivamia nyumba moja katika eneo hilo iliyokuwa katika maombolezi na kuwataka kuzima nyimbo zilizokuwa zikiendelea. Alidai kuwa nyimbo hizo zilikuwa zikifanyia familia yake makelele.

You can share this post!

Watoto zaidi ya 2,000 waambukizwa HIV kwa kunyonyeshwa

400 wafa vita kati ya Israeli na Wapalestina vikichacha