• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Wavukaji feri kuendelea kulipia kupitia kwa Mpesa

Wavukaji feri kuendelea kulipia kupitia kwa Mpesa

Na PHILIP MUYANGA

WATUMIAJI wa kivuko cha feri cha Likoni, Kaunti ya Mombasa, wataendelea kulipia ada za kuvuka kupitia kwa Mpesa hadi kesi ya kupinga mfumo huo itakapoamuliwa.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Muslims for Human Rights (Muhuri) lilikuwa limeomba mahakama kusitisha mfumo huo hadi kesi yake ya kuupinga itakapokamilika.

Jaji Eric Ogola aliamua kuwa Muhuri haijafafanua wazi kuhusu haki inazodai zinakiukwa.

Shirika la Huduma za Feri nchini (KFS) lilikuwa limetetea utumizi wa Mpesa kupokea ada za magari kuvuka feri na kusema ulinuiwa kutimiza mwongozo wa serikali kuu unaohimiza mashirika kutopokea pesa taslimu wakati wa utoaji wa huduma.

KFS ilisema serikali ilitangaza mwongozo huo kama sehemu za mbinu za kuepusha ueneaji wa virusi vya corona.

Zabuni ya kukusanya ada hizo ilipeanwa kwa kampuni ya Safaricom na Benki ya National mnamo Mei, 2020.

Kulingana na Muhuri, hakuna mwendeshaji gari yeyote ambaye hukubaliwa kuvuka feri kama hana uwezo wa kulipia ada inayohitajika kupitia Mpesa pekee.

Shirika hilo lilishtaki KFS, Waziri wa Uchukuzi na Miundomsingi, na Mwanasheria Mkuu likitaka watumiaji wa feri wakubaliwe kutumia mbinu nyingine za kulipia ada ikiwemo pesa taslimu na kupitia kwa mifumo mingine ya malipo ya kidijitali.

You can share this post!

Watoto wa marais wakwama na Raila

Wakazi walia daraja bovu na ahadi hewa