• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Wazazi walee watoto wao ipasavyo kwani ni amana kutoka kwa Mungu

Wazazi walee watoto wao ipasavyo kwani ni amana kutoka kwa Mungu

SIFA zote njema anastahiki Mola Azzawajalla, Mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na nyingine ndogondogo.

Swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, rahmatan lil ‘alamiyn, maswahaba wake kiram na watangu wema hadi siku ya Kiyaamah. Sheria ya Kiislamu imewaamuru wazazi kuwa ni dhamana kwa maisha ya mtoto na makuzi yake.

Kwa msingi wa kwamba, mtoto huchukuliwa kuwa ni dhamana waliyopewa, ambayo inapaswa kutunzwa nao kwani watakujaeleza mbele ya Mwenyezi Mungu (jinsi walivyoitunza amana waliyopewa).Mtoto mwanzoni mwa maisha yake huwa hajui hatari hasa ambazo zingehatarisha maisha yake.

Kwa kuongezea ni kwamba yeye hawezi kujilisha na kuchunga maisha yake, kwa hivyo basi, ndipo Mwenyezi Mungu akawafanya wazazi kuwa ni dhamana kwa ajili ya kuwalinda watoto wao kutokana na magonjwa mbalimbali na hatari ambazo zingetishia maisha na makuzi yao.

Imetajwa katika Hadith: “Kila mmoja wenu ni mchungaji na kila mmoja ataulizwa juu ya kile akichungacho. Baba ni mlezi wa jamii yake. Mke ni mchungaji wa mali ya mumewe na watoto wake, na ndiye atakayeulizwa kuhusu akitunzacho.

Mtumishi ni mtunzaji wa mali ya tajiri yake na ndiye atakayeulizwa kuhusu mali aitunzayo. Ndiyo, kila mmoja wenu ni mchungaji na ndiye atakayeulizwa juu ya anachokiangalia.”? Mbali na kuwa ni dhamana, ni wajibu wao pia kuwalisha watoto wao na kuwatoshelezea mahitaji yao, hii inaweza kuwa kwa kuwachagulia kwa njia nzuri chakula chao, na kuwalinda kutokana na maradhi yote yatakayowadhuru.

Miongoni mwa hatari zinazoweza kutishia maisha ya mtoto katika miaka yake ya mwanzoni ni uwezekano wa kupatwa na mojawapo ya maradhi yauwayo watoto kama:Ugonjwa wa kupooza (Polio), Surua (Ukambi), dondakoo (DPT au Diphtheria) n.k. Au upungufu wa maji mwilini uletwao na magonjwa ya kuharisha n.k.

Magonjwa hayo yote yanaweza kumshambulia mtoto, kumlemaza na kumhuzunisha maisha yake na ya wazazi wake.Uislamu unatuonya vikali sana tusipuuze matunzo na matibabu ya watoto wetu kutokana na maradhi yauwayo watoto au mengineo. Kwa ajili hiyo, Uislamu unaamrisha waumini wake kuwa wenye nguvu na afya.

Mtume (s.a.w.) amesema: “Muislamu mwenye nguvu ni bora na ndiye apendezaye zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko Muislamu mnyonge.’’Kwa kuwa upendo wa wazazi kwa watoto ni sehemu ya maumbile yao (wazazi) ya kiasili, ndipo ikawa hapana haja ya kuagizwa juu ya jambo hilo, kwa hivyo Uislamu umetilia mkazo zaidi umuhimu wa ‘matunzo’ ya watoto na ukaonya vikali wazazi wasizembee katika jambo hilo, ili familia na jamii ziweze kuishi kwa raha na furaha.

Na hii hatimaye huleta muundo wa kizazi ambacho kitategemewa kuweza kubeba mzigo wake barabara na katika hali ya kujitegemea.Imetajwa katika Qur’ani: “Wala msijitie wenyewe katika maangamivu.” (2:145).

Na je ni maangamivu gani maovu zaidi ambayo mtu anaweza akajifanyia mwenyewe kuliko kuingiza kiwiliwili chake na damu (watoto) wake kwenye hatari ya kifo na adhabu? Imetajwa tena katika Qur’ani: “Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu (jamii) wenu kutokana na moto, ambao kuni zake ni watu na mawe….”(66:6)Kujilinda na maangamivu (ya ugonjwa n.k.) kuna maana sawa na kuna daraja moja na kuilinda jamii kutokana na maangamivu ya motoni.

Ikiwa kujilinda kunahitajika kwa ajili ya maisha ya akhera, basi kujilinda huko kunahitajika zaidi wakati wa maisha ya duniani kwani kile ukipendacho katika maisha yako duniani ndicho utakachokivuna akhera.Kujilinda kwa maana hiyo, hakumaanishi kujizuia kutokana na kutenda maovu, madhambi na mambo ya fedheha tu, bali ina maana ya ndani zaidi kuhusiana na usawa baina ya mahitaji ya nafsi, kiwiliwili, roho, na kujilinda na maneno ya Mtume (s.a.w.) aliposema: “Yatosha kwa mtu kupata dhambi kwa kutomjali yule anaemtegemea.

” Pia: “Nyote ni wachungaji na kila mmoja wenu ataulizwa kutokana na kile anachokichunga.”Tukizingatia, inatudhihirikia wazi kwamba kuwakinga watu wetu kutokana na maradhi ni amri ya kidini na ni wajibu wa jamii na pia ni wajibu wa taifa zima.

Mtume (s.a.w.) amesema: “Mwenye kuitunza jamii na hakuipa nasaha (maonyo), basi mtu huyo atanyimwa pepo.”Na mwishowe ataokoka Siku ya Kiyama kutokana na vitisho ambavyo vingempata wakati Mwenyezi Mungu atapomuuliza kuhusu hali ya wafuasi wake (wenye kumtegemea) na sababu ya kuwa mzembe katika jambo hilo.

Kwa hivyo basi, iwapo wazazi hawatachukua hatua zifaazo ili kulinda maisha ya watoto wao kuwakinga kutokana na maradhi, kuna uwezekano mkubwa wa kunyimwa pepo akhera

  • Tags

You can share this post!

Ronaldo afikia rekodi ya ufungaji bora wa mabao kimataifa

Man-United kuvunja benki kwa ajili ya Sancho