• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 7:50 AM
Man-United kuvunja benki kwa ajili ya Sancho

Man-United kuvunja benki kwa ajili ya Sancho

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

MANCHESTER United wameongeza ofa yao kwa ajili ya huduma za chipukizi Jadon Sancho hadi Sh11.3 bilioni.

Hii ni baada ya ofa yao ya awali ya Sh9.4 bilioni kwa ajili ya fowadi huyo raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 21 kukataliwa na klabu ya Borussia Dortmund ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Sancho kwa sasa ni sehemu ya kikosi cha Uingereza kinachoshiriki kipute cha Euro. Sogora huyo amefungia Dortmund mabao 50 kutokana na mechi 137 na amepachika Uingereza magoli matatu kutokana na mechi 20.

Katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita, Sancho amehusika katika mabao 109 ambayo yamefungwa na Dortmund na akacheka na nyavu mara mbili waliposhinda RB Leipzig kwenye fainali ya German Cup mnamo Mei 2021.

Man-United walikosa kujinasia maarifa ya Sancho miezi 12 iliyopita baada ya Dortmund kuwawekea bei ya Sh16.8 bilioni. Sancho alijiunga na Dortmund mnamo Agosti 2017 baada ya kuagana na Manchester City kwa Sh1.5 bilioni.

Kufaulu kwa mpango huo wa kusajiliwa kwa Sancho kutamfanya awe mchezaji wa pili ghali zaidi kuwahi kutua Old Trafford baada ya kiungo Paul Pogba kusajiliwa na Man-United kwa kima cha Sh12.4 bilioni kutoka Juventus ya Italia mnamo 2016.

Chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer ambaye ni raia wa Norway, Man-United waliweka mezani kima cha Sh11.2 bilioni ili kumshawishi beki na nahodha Harry Maguire kuagana na Leicester City ugani King Power miaka miwili iliyopita.

Dortmund wako radhi kumwachilia Sancho aondoke uwanjani Signal Iduna Park ili wasalie na fowadi raia wa Norway, Erling Halaand anayemezewa pia na Manchester City ambao wanatafuta mfumaji mrithi wa Sergio Aguero aliyeyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Barcelona.Man-City na Man-United wanamhemea pia fowadi na nahodha wa Tottenham Hotspur, Harry Kane.

Ili kuwatamausha Man-City kunaomfukuzia Haaland, Dortmund wamefichua kwamba bei mpya ya fowadi huyo wa zamani wa RB Salzburg ni Sh19.6 bilioni. Man-City waliokuwa waajiri wa zamani wa Sancho watatia kapuni bonasi ya Sh1.5 bilioni iwapo kiungo huyo mvamizi atatua Man-United.

  • Tags

You can share this post!

Wazazi walee watoto wao ipasavyo kwani ni amana kutoka kwa...

Ujerumani kuvaana na Uingereza kwenye hatua ya 16-bora ya...