• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:50 AM
Wazee na wachungaji wabishania tohara ya vijana wa Agikuyu

Wazee na wachungaji wabishania tohara ya vijana wa Agikuyu

NA MWANGI MUIRURI 

WAZEE wa Agikuyu pamoja na viongozi wa kidini wameungana kuchora jinsi makanisa yatakomeshwa kuendesha tohara ya wanaume katika jamii hiyo.

Mshirikishi wa mpango huo Bw Joseph Kaguthi alisema kwamba wanalenga kuwa wamezima tohara hiyo ya kanisa kabla ya 2027.

“Makanisa yamekuwa yakiendesha tohara ya vijana wetu wa kiume kama biashara. Hali hiyo imeteka nyara suala muhimu la kitamaduni na kuligeuza kuwa sarakasi,” akasema katika Mkahawa Mjini Murang’a.

Bw Kaguthi alisema kwamba “kwa sasa tohara katika jamii ya Agikuyu imekosa maana kwa kuwa hata kuna wanawake ambao huwapeleka vijana wao wa kiume kutahirishwa na kisha kuwanyima ushauri nasaha wa kimaisha kama madume wa kijamii”.

Hata hivyo, baadhi ya makundi ya kijamii yamepinga vikali hatua hiyo ya wazee ya kuweka masharti ya jinsi vijana wa kiume watapashwa tohara.

“Udhibiti wa tohara uliwatoka walifanya nini? Hospitali ndizo zilikuwa za kwanza kutwaa hafla hiyo baada ya watahirishaji wa kitamaduni kufifia. Kisha kanisa ikaingilia kati ili kutwaa nafasi ya kutoa ushauri wa kidini kwa vijana hao,” akasema Bi Charity Mutugi ambaye ni mshirikishi wa vuguvugu la wanawake waelimishaji (Fawe).

Bi Mutugi alisema kwamba kanisa lilitwaa wajibu huo baada ya itikadi za utamaduni kutwaliwa na magenge hatari kama Mungiki.

“Mtoto ni wangu sio wa wazee hawa. Hutaniambia nikupe mtoto wangu ukatahirishe halafu umrejeshe kwangu akiwa amesajiliwa katika ujambazi. Tutazidi kuwapeleka kanisani wakapashwe tohara huku wakipewa mawaidha ya kidini,” akasema.

Aliwataka wazee hao kwanza wajipige msasa na wajiulize ni kwa nini hata kina mama wa kijamii huwa hawawachukulii kwa uzito unaowafaa.

“Hawana hata umoja na tunachoona ni siasa za migawanyiko. Hawapendani, hawana umoja na hawana msimamo wa dhati. Vile wamechanganyikiwa wasitake kusambazia vijana wetu migawanyiko hiyo,” akasema.

Hata hivyo, Bw Kaguthi alisema kwamba “huo ni mchango mzuri wa pingamizi na ambao utatumika kulainisha mjadala huo wa kijamii ili kuzidisha nafasi ya kuafikiana kuhusu suala hilo muhimu”.

Alisema kwamba wazee na wachungaji wataingia kwenye mkataba wa maelewano kuhusu suala hilo la tohara “kwa kuwa hatuwezi tukapuuza mila na desturi na vile vile hatuwezi tukapuuza nafasi ya dini katika jamii”.

 

  • Tags

You can share this post!

Viongozi, maafisa wa kiusalama Mlima Kenya walia...

Miguna Miguna akosa kwenye orodha ya uteuzi wa DPP

T L