• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Viongozi, maafisa wa kiusalama Mlima Kenya walia ‘kurambwa’ na udikteta serikalini 

Viongozi, maafisa wa kiusalama Mlima Kenya walia ‘kurambwa’ na udikteta serikalini 

NA MWANGI MUIRURI

BAADHI ya viongozi wa kisiasa na wa kiusalama Mlima Kenya wanalalamikia utawala wa kidikteta, ubaguzi na ukandamizaji ambapo tofauti inapoibuka na ‘mkubwa fulani serikalini’, wanaanza kuhangaishwa.

Wa kwanza kupiga nduru hali si shwari eneo hilo ni mbunge wa Laikipia Mashariki, Bw Mwangi Kiunjuri ambaye Mei 2023 alisema “hii serikali ya Kenya Kwanza ina mkono na mdomo wa ukandamizaji”.

Alitangaza kuwa “kunao ambao wamekuwa wakitupigia simu wakituonya dhidi ya kuzindua kampeni za kudai usawa wa ugavi wa rasilimali na vyeo almaarufu one man one shilling one vote“.

Bw Kiunjuri alisema kwamba “hao ni wale ambao wanadhania watakuwa wasemaji wa Mlima kwa kukandamiza wengine”.

Punde tu baada ya kutangaza hayo, Mbunge wa Githunguri Bi Gathoni wa Muchomba alitangaza kwamba “nilipoanza harakati za usawa huo, nilikemewa na kuambiwa nimeanza mbio mapema na nilipaswa kunyamaza”.

Alipojitokeza hivi majuzi kupinga Mswada wa Kifedha wa 2023, Bi Wa Muchomba alikumbana na upinzani mkali kiasi kwamba hasidi wake wa kisiasa Bw Kago wa Lydiah alianza kufadhiliwa kuwakilisha serikali katika eneobunge la Githunguri.

Mbunge wa Mathira, Bw Eric wa Mumbi alikuwa miongoni mwa wengine waliokuwa wametangaza kupinga mswada huo tata lakini haikujulikani alivyobadilisha msimamo wake.

Katika mawimbi ya mkono wa ukandamizaji, baadhi ya magavana, maseneta na wabunge wamegeuzwa kuwa vibarakala wa kuitikia tu lisemwalo.

“Mimi nilifikiria kwamba viongozi huwa na msimamo wao wa masuala nchini na wana uhuru wa kuchangia maoni…Hadi wakati ule nilinukuliwa na vyombo vya habari nikisema Mlima ulifaa msemaji mbadala,” akasema mmoja wa viongozi eneo hilo.

Anasema kuwa “Kuna kiongozi wa kusambaza hofu, uoga na wasiwasi ambaye aliamrisha afisi yangu inyimwe marupurupu na hata pesa za gharama za kila siku na hali ilirudi kawaida baada ya kuamrishwa niombe msamaha na nikariri kwamba yeye ndiye alikuwa kinara wa siasa za Mlima Kenya “.

Hata maafisa wa kiusalama hawajaachwa nyuma katika mahangaiko hayo ambapo kunao wamezimwa kupandishwa mamlaka kwa msingi kuwa sio watiifu kwa mwanasiasa huyo.

“Nimepata habari kwamba huko Murang’a kuna afisa amehamishwa kwa kudhaniwa kuwa na utiifu kwa Waziri wa Usalama Prof Kithure Kindiki…Amesema kuwa katika mrengo wa wengine ambao wanahujumu mrengo unaodhaniwa kuwa na usemi mkuu ndani ya Kenya Kwanza,” akasema aliyekuwa mbunge wa Maragua Bw Elias Mbau.

Afisi ya Murang’a ya afisa huyo imeletwa mwingine aliyetimuliwa mwaka jana baada ya kuhusishwa na kashfa ya mashamba na ambapo kikao kimoja chake kilirushiwa gesi ya kutoa machozi kukisambaratisha.

Afisa huyo alihamishiwa hadi eneo la Kaskazini Mashariki, akiwa msaidizi wa mkuu wa eneo hilo lakini sasa, katika hali isiyokuwa kanuni na utaratibu, amerejeshewa wadhifa wake aliopokonywa baada ya kuhudumu kwa miaka minne.

Ni vivyo hivyo kwa afisa mwingine wa kiwango cha Naibu Kamishna ambaye hivi majuzi alipandishwa ngazi hadi kuwa Kamishna wa Kaunti.

Mnamo Aprili 20, 2023 afisa wa polisi Murang’a alishutumiwa kwa madai kwamba alimsaidia kinara wa Azimio Bw Raila Odinga kuandaa mkutano kukemea serikali katika ukumbi wa Mother’s Union.

Baadaye, alipewa uhamisho hadi Bonde la Ufa kama adhabu ya kutotii kinara wa Mlima Kenya ambaye alikuwa ameamrisha asikubaliwe kufika.

Siasa hizo za ukandamizaji na kuogofya ndizo zinasemwa kuzua mitafaruku katika eneo la Mlima Kenya ambapo wabunge wanatusiana hadharani, mawaziri wanasambaza matusi ili kuwakemea wanaoonekana kutotii kinara huyo huku wengine wakinyamazishwa kama amri ya mwalimu ifanyavyo kwa watoto wa shule.

 

  • Tags

You can share this post!

Masaibu: Bloga wa Azimio Pauline Njoroge akamatwa kwa madai...

Wazee na wachungaji wabishania tohara ya vijana wa Agikuyu

T L