• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 6:55 AM
Wazee wa vijiji kutambuliwa rasmi kisheria

Wazee wa vijiji kutambuliwa rasmi kisheria

NA MARY WANGARI

WAZEE wa vijiji ambao wamekuwa wakijituma kuimarisha usalama mashinani bila malipo huenda hatimaye wakatambuliwa rasmi kama maafisa wa umma, kwa mujibu wa Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki.

Hata hivyo, wazee hao wapatao zaidi ya 70,000 watalazimika kusubiri huku serikali ikianzisha mikakati ya kisheria na kisera ili kutoa mwongozo thabiti kuhusu hatua hiyo.

Akizungumzia Alhamisi mbele ya Seneti kuhusu Kuwatambua Wazee wa Vijiji na Malipo yao chini ya Mpango wa Nyumba Kumi, Waziri Kindiki alikiri kwamba kwa sasa hakuna sera inayowatambulisha rasmi wazee wa kijiji kama maafisa wa umma.

Kamati ya Seneti kuhusu Usalama wa Kitaifa, Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni inayoongozwa na Seneta wa Baringo William Cheptumo ilisikia kwamba kwa sasa sheria inatambua hadi kufikia ngazi ya manaibu wa machifu katika mfumo wa usimamizi.

Kenya ina takriban kaunti ndogo 9,045 zinazokadiriwa kuwa na jumla ya vijiji vinane kila kaunti ndogo, kumaanisha kuna wazee wa kijiji wapatao 72, 360 wanaotumikia umma kwa kuimarisha usalama katika kaunti mbalimbali kote nchini.

“Wazee wa kijiji na Nyumba Kumi wote ni wahudumu wa kujitolea bila malipo. Kwa sasa hatuna sera thabiti kuhusu suala hilo. Mchango wa wazee wa Vijiji ni muhimu na unapaswa kutambuliwa rasmi kupitia sheria,” alisema Waziri Kindiki.

Waziri alisema serikali kwa ushirikiano na wadau mbalimbali ikiwemo Tume ya Mishahara (SRC) na Hazina Kuu imeanzisha mikakati ya kubuni mwongozo kuhusu jinsi ya kuwashirikisha wazee wa kijiji.

“Marekebisho ya kisheria yanahitajika ili kufafanua kuhusu jinsi watakavyoshirikishwa, malipo yao, jinsi watakavyoteuliwa, mchakato wa kuwaachisha kazi, masharti ya kujiondoa afisini, hatua za kinidhamu kwa watakaopotoka kisheria ikiwemo jinsi ya kuunda vijiji,” alisema.

Waundasheria wakiongozwa na Seneta wa Pokot Magharibi, Julius Murgor walitaka kujua endapo wazee wa kijiji watakuwa chini ya serikali kuu au za kaunti.

Sheria ya Serikali za Kaunti 2012 inatambua Utawala wa Vijiji ambapo wazee wa kijiji na baraza la wazee wanatambuliwa ikiwemo taratibu za kuwalipa ambapo Waziri alifafanua kuwa sheria hizo zitaoanishwa ili kutoa utaratibu wazi.

Waziri hata hivyo alipendekeza wazee wa vijiji kulipwa kiasi fulani cha pesa kati ya Sh500 to Sh1,000 kama ishara ya shukrani wanapohudhuria vikao ili kuwawezesha kujikimu kimaisha huku akirejelea gharama ya juu ya maisha.

“Gharama ya mishahara ipo juu mno ilihali haya ni masuala muhimu ambayo hayawezi kupuuzwa. Njia mojawapo ni kuwaangazia wazee hawa na kuwawezeshwa kulipwa kwa kuwashirikisha kwa muda na kuwapa marupurupu au kuwajumuisha kikamilifu,” akasema.

Profesa Kindi alifafanua kwamba kwa kuwa “Wizara za Usalama na Ulinzi zimeorosheshwa chini ya Serikali Kuu, Wazee wa Vijiji watakuwa sehemu ya mfumo wa serikali kuu kwa sababu kitengo cha usalama hakijaorodheshwa chini ya serikali za kaunti”.

  • Tags

You can share this post!

Aliyeangushwa ashtakiwa kwa kutishia kumuua diwani

AAR kutoa huduma za afya katika eneo pana la Tatu City

T L