• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Wenye ardhi inayohusishwa na Ruto Laikipia hawajulikani

Wenye ardhi inayohusishwa na Ruto Laikipia hawajulikani

Na DENNIS MATARA

ARDHI ya ADC Mutara, Kaunti ya Laikipia ambayo imehusihwa na Naibu Rais William Ruto, imekodishwa kwa watu kadhaa baadhi ambao majina yao ni siri kubwa.

Kulingana meneja mmoja wa shamba hilo kubwa, Benard Maranga, ADC, ambalo ni shirika la serikali linamiliki ardhi hiyo lakini imekodisha sehemu kwa watu wanaoendesha shughuli tofauti.

“ADC imekodisha sehemu ya ardhi kwa watu ambao wanashiriki kilimo. Sehemu iliyobaki inasimamiwa na ADC,” alifichua Maranga.

Taifa Leo ilibaini kuwa baadhi ya wanaomiliki ardhi iliyo ndani ya shamba la ADC Mutara ni Bw Musa Haji na Mark Powsy, Mkenya mwenye asili ya Uingereza.

Wawili hao wanashiriki kwa kufuga mifugo na kupanda mimea.

Majina ya wamiliki wengine hayajulikani na juhudi za kupata majina yao hazikufua dafu.

Sehemu kubwa ya ardhi ina ng’ombe aina ya Boran ambao mfanyakazi mmoja alikadiria kuwa zaidi ya ekari 6,000.

Kuna sehemu iliyo na shamba kubwa la mahindi linaloonekana kutoka barabara ya Nanyuki-Rumuruti.

Wafanyakazi waliohojiwa walisema wamiliki wa sehemu iliyokodishwa hawajulikani na wamesalia kuwa siri.

“Ninajua baadhi ya watu wamekodisha sehemu ya ardhi, lakini sijui majina yao. Ni wasimamizi wa ADC na serikali wanaojua wanaomiliki ardhi hiyo. Hata hivyo, nawajua wawili,” mfanyakazi mmoja aliyeomba tusitaje jina alisema.

Wafanyakazi hao walisema hawajawahi kumuona Dkt Ruto katika ardhi ya ADC Mutara.Ingawa wasimamizi wanakataa kutaja majina ya watu waliokodisha ardhi katika shamba hilo, kumekuwa na madai kuwa Dkt Ruto anamiliki ekari 15,000.

Mapema mwezi huu Septemba, waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’i alifichua kuwa Dkt Ruto anamiliki maelfu ya ekari katika shamba la ADC Mutara anakofuga ng’ombe na kupanda mahindi.

Naibu Rais amekanusha madai hayo akisema ni uongo.

Ijapokuwa Taifa Leo ilibaini kuwa Dkt Ruto hajawahi kuonekana katika shamba hilo, haikuweza kubaini ikiwa anamiliki sehemu ya ardhi kupitia watu wengine.

Dkt Matiang’i alifichua kwamba afisa mkuu wa serikali anayemiliki sehemu ya shamba hilo ni Naibu Rais William Ruto.

You can share this post!

Matokeo mseto Kenya ikianza ndondi za majeshi nchini Urusi

Pendekezo barabara ya jiji la Nairobi ipewe jina la Raila