• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Matokeo mseto Kenya ikianza ndondi za majeshi nchini Urusi

Matokeo mseto Kenya ikianza ndondi za majeshi nchini Urusi

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imeandikisha matokeo mseto kwenye mashindano ya ndondi ya dunia ya wanajeshi baada ya Samuel Njau Wairimu kutwaa ushindi naye Washington Wandera Wabwire akapoteza jijini Moscow nchini Urusi mnamo Septemba 20.

Njau alikuwa wa kwanza kushuka jukwaani katika mashindano hayo yaliyovutia mabondia 66 kutoka mataifa 25.

Akicheza katika kitengo cha uzani wa kilo 56, Njau aliibuka mshindi dhidi ya Lauruschyk Aleksandr kutoka Belarus kwa wingi wa pointi na kuingia robo-fainali.

Wandera hakuwa na lake dhidi ya Abdurasulov Shunkor kutoka Uzbekistan akibanduliwa katika uzani wa kilo 60 katika ukumbi wa CSKA Igrovoy.

Kenya pia inawakilishwa katika mashindano hayo na Fredrick Ramogi Otieno (uzani wa zaidi ya kilo 91), Fredrick Onyango Walter (kilo 91), Chrispin Murimi (kilo 69), Kelvin Michira Maina (kilo 52) na Abednego Kyalo (kilo 46-49) pamoja na mwanadada Pauline Wandia Chege (kilo 57).

Ramogi ameratibiwa kuanza kampeni yake dhidi ya Ashish Duwadi (Nepal), Abednego kupepetana na Muhammad Saeed (Pakistan), Maina kupigana na Juliano Fernando Gento Maquina (Msumbiji), Murimi kulimana na Dan Bahadur Darlami (Nepal), Onyango kuangushiana makonde na Michel Erpelding (Luxembourg) na Chege dhidi ya Bolortuul Tumurkhuyag (Mongolia).

Mataifa yanayoshiriki ni Algeria, Armenia, Azerbaijan, Bangladesh, Belarus, Brazil, DR Congo, Ufaransa, Ireland, Italia, Kazakhstan, Mongolia, Msumbiji, Nepal, Pakistan, Poland, Korea Kusini, Congo Brazzaville, Yemen, Urusi, Sri Lanka, Syria, Tunisia, Uzbekistan na Venezuela.

You can share this post!

Wachungaji kutoka Thika Mashariki watakasa eneo la mauti

Wenye ardhi inayohusishwa na Ruto Laikipia hawajulikani