• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
Ajivunia kuwa askari wa kaunti baada ya kiwango cha elimu kumnyima fursa jeshini

Ajivunia kuwa askari wa kaunti baada ya kiwango cha elimu kumnyima fursa jeshini

NA KALUME KAZUNGU

TANGU utotoni mwake, ndoto kuu kwa Omar Harun Musa ilikuwa kwamba siku moja atumikie kikosi cha Jeshi la Ulinzi la Nchi Kavu Kenya (KDF).

Harun,31, ambaye alizaliwa Kisiwa cha Kizingitini, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki, anasema mapenzi yake makuu ya kuhudumia kikosi cha KDF yalimfanya mara nyingi kujipata akizama kwenye bahari ya luja, akiwaza na kuwazua usiku na mchana jinsi ambavyo atatekeleza kikamilifu jukumu lake la kuilinda Jamhuri ya Kenya, kudumisha amani ya kimataifa au hata kushiriki misheni za ulinzi na amani kwenye maeneo kama vile Kismayo nchini Somalia na migogoro mingineyo endapo siku moja ndoto yake itaibuka kuwa kweli.

Ama kwa hakika, ‘Kipendacho Moyo Dawa’.

Ili kuona kwamba anafaulisha malengo yake, Bw Harun alianza jitihada za mapema masomoni, akidurusu madakftari yake kwa bidii mithili ya mchwa punde alipojiunga na Shule ya Msingi ya Mokowe iliyoko Lamu Magharibi.

Baada ya kuhitimisha masomo yake ya msingi na kupasi vyema mnamo 2010, Bw Harun alianza kushuhudia mambo yakimwendea mafyongo kwani ufukara wa familia yake ulimzuia yeye kujiunga na shule ya sekondari ili kuendeleza kisomo chake.

Alijaribu kuzuru ofisi tofautitofauti kote Lamu kuomba ufadhili wa karo lakini wapi.

Kila alipobisha hodi kuomba msaada, tumaini lilizidi kujitenga mbali naye mfano wa ardhi na mbingu.

Bw Omar Harun Musa,31, ambaye ni askari wa Kaunti ya Lamu, alinda lango kuu la ofisi za Baraza la mji wa Lamu. Baada ya miaka mingi ya kutafuta nafasi ya kuajiriwa jeshini (KDF), Bw Harun alipiga moyo konde kufanya kazi hii ambayo anajivunia pakubwa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Utandu na kiza cha kaniki kikatanda mbele yake.

Hapo ndipo Bw Harun alipiga moyo konde..Potelea mbali…Akajitosa mzimamzima katika kazi za vijungujiko mitaani ilmradi ayafanikishe maisha yake

Licha ya kisomo chake kukatizwa hivyo, Bw Harun hakufa moyo.

Aliendelea kuipalilia ndoto yake kwamba siku moja awe afisa wa KDF, ambapo alitenga muda wa kushiriki mazoezi, ikiwemo mbio ilmradi auweke mwili wake sawasawa kisiha.

Bw Harun pia alikuwa akitegea kila wakati kunapotangazwa tarehe ya shughuli ya kusajili makurutu Lamu, ambapo angebeba stakabadhi zake, ikiwemo cheti chake cha mtihani wa kitaifa kwa darasa la nane (KCPE), ambapo angejitokeza pale na kukabidhi hati hizo wahusika, akijua fika kwamba hatoshi mboga kimatakwa yanayohitajika kwa kurutu kupata nafasi hiyo adimu ya kusajiliwa jeshini.

Baada ya mara zisizopungua kumi za kujaribu bahati yake ya kusajiliwa jeshini, haikusimama.

Akasalimu amri kwamba kisomo chake ndicho kilichotia doa jeusi njozi yake ya kuwa mwanajeshi.

Akazinduka usingizini.

“Hapo ndipo nilipojua fika kuwa licha ya nafsi yangu kunisukuma niwe mwanajeshi lakini kisomo changu finyu kiliniponza. Kila nilipofika ugani kutaka kushiriki mbio na kusajiliwa kuwa KDF, niliitishwa stakabadhi zangu na nilikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kwanza kutolewa folenini kutokana na kisomo changu cha chini,” anaeleza Bw Harun.

Mwishowe alipiga moyo konde na kubadili fikra zake kuhusu mustakabali wa maisha yake ya mbeleni.

“Nilianza kujihusisha na utoaji huduma za bure, hasa kwa maofisi mbalimbali hapa Lamu. Mnamo 2013 baada ya serikali za ugatuzi kutwaa hatamu, nikaomba nafasi ya kuhudumia jamii yangu ya Lamu kwa kujitolea bila malipo hasa katika kitengo cha ulinzi (askari wa kaunti). Nikakubaliwa,” akasema Bw Harun.

Anasema aliifanya kazi hiyo ya askari wa kaunti kwa moyo safi, ukamilifu na kwa muda mrefu.

Bw Omar Harun Musa akiwa ofisini mwake kwenye lango kuu la kuingia kwa ofisi za baraza la mji wa Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kwenye sherehe mbalimbali, iwe ni za kijamii au kitaifa, ulikuwa ukimpata Bw Harun mbelembele, akiwa amesimama tisti na fimbo yake au akiweka ulinzi na kuwapanga waja huku akiwazungumzia kwa ukarimu na upole.

Hali hiyo ilimzolea umaarufu na kuibuka kupendwa na kuheshimiwa na wengi ila wasichokijua ni kwamba afisa huyo hakuwa analipwa chochote bali ni wakujitolea mhanga na kujisimamia mwenyewe tu.

“Nilifanya jukumu langu kwa moyo mkunjufu kiasi kwamba gavana wetu wa Lamu Issa Timamy akanitambua kwa nilivyojitolea. Hapo ndipo akaniajiri rasmi kama miongoni mwa askari wa kaunti ya Lamu japo kwa kandarasi,” akaeleza Bw Harun.

Anasema tangu alipoajiriwa, yeye katu hajuti tena kwani kila anapovalia magwanda ya askari wa kaunti ya Lamu nafsi yake hujihisi ikitekeleza jukumu ambalo lilikuwa ni ndoto ya udogoni mwake.

Bw Omar Harun Musa,31, akilinda ofisi za baraza la mji wa Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Miongoni mwa majukumu yake ya sasa ni kulinda ofisi za baraza la mji wa Lamu na pia kuhakikisha usafi na mpangilio bora kwenye sehemu ya mbele ya mji wa kale wa Lamu.

Anasema kutokana na ari yake ya kazi, yeye hudamka kuanza shughuli majira ya saa kumi unusu alfajiri na kurudi nyumbani saa kumi na mbili jioni.

“Japo sikufaulu kuingia kwenye kikosi cha KDF, lakini bado nina furaha kwamba ninafanya kazi inayooana kidogo na hiyo ya jeshi. Kila nikivalia magwanda ya askari wa kaunti na kusimama kwenye lango kuu kulinda, bado najihisi mwanajeshi kamili japo natekeleza majukumu yangu kwa namna nyingine,” anasema Bw Harun.

Kwa sasa ameelekeza fikra zake katika kutia bidii kazini na kuhakikisha anasomesha vyema wanawe ili siku moja mmoja wa watoto hao ajiunge na jeshi (KDF) bila ya kikwazo chochote, hasa kile kinachohusiana na masomo kama ilivyomkumba.

“Ni matumaini yangu kwamba licha ya mimi mwenyewe kisomo kunikosesha nafasi ya kutumikia nchi yangu kama afisa wa KDF, mmoja wa wanangu ajiunge na kikosi hicho. Hilo likitimia siku moja basi itakuwa hiyo ndiyo siku njema kwangu,” akasema Bw Harun.

Bw Harun alizaliwa kijijini Kizingitini mnamo Juni 11, 1992, na kukulia mjini Mokowe baada ya wazazi wake kuhamia eneo hilo.

Ni mzawa wa tatu katika familia ya watoto watano, ikiwemo wavulana watatu na wasichana wawili.

Ameoa na ni baba wa watoto wawili wa mama mmoja.

  • Tags

You can share this post!

Harry Kane aanza kampeni ya Bundesliga kwa matao ya juu

Kuria akaangwa kwa kutaka ushuru wa mitumba upandishwe hadi...

T L