• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
Mbinu ya kijamii inayotumika Pokot Magharibi kuzima ukeketaji, visa vikiripotiwa kupungua 

Mbinu ya kijamii inayotumika Pokot Magharibi kuzima ukeketaji, visa vikiripotiwa kupungua 

NA OSCAR KAKAI

KAUNTI ya Pokot Magharibi imeandikisha kupungua kwa visa vya ukeketaji, hasa maeneo ya mashinani kufuatia kampeni inayoendelezwa na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa ushirikiano na wenyeji.

Uchunguzi unaonyesha maeneo ya mpaka wa Kenya -Uganda, visa hivyo vya dhuluma kwa wasichana na wanawake vimepungua.

Kulingana na ripoti ya afya ya mwaka wa 2022, visa vya ukeketaji vimepungua kutoka asilimia 38 mwaka wa 1998 hadi asilimia 15 mwaka wa 2022, na kutoka asilimia 21 mwaka wa 2014.

Kitaifa, Pokot Magharibi inawakilishwa na asilimia 74 ya visa hivyo.

Upungufu ulioandikishwa, unatokana na mbinu mpya ambazo zimeletwa na mashirika ya kijamii ambayo yanapambana na maovu hayo.

Community Change, ni mojawapo ya mifumo ya hadithi za ufanisi inayotumika kuhamasisha vita dhidi ya ukeketaji na ndoa za mepema miongoni mwa wasichana.

Eneo moja ambapo mfumo huo unafanya kazi vyema ni Alale, eneo ambalo linapakana na nchi jirani ya Uganda ambalo lilikuwa na visa vingi vya ukeketaji na ndoa za mepama.

Mfumo huo mpya unaofadhiliwa na World Vision, unatumika kupigana na visa potovu vilivyopitwa na wakati vya ukeketaji na ndoa za mapema kati ya wasichana wadogo na kuendeleza elimu katika vijiji mashinani.

Aidha, mfumo huo unahusisha wanachama wa jamiii kupewa mafunzo na wahamasishaji wa jamii kubadilisha fikra za wakazi, jambo ambalo limesaidia ngariba sugu kusamilisha visu vyao.

Zaidi ya watoto 300 wamerejea shuleni, na makundi ya kibinafsi kubuniwa ili kuimarisha vitega uchumi vya wakazi ambao wameasi maovu hayo.

Hali kadhalika, zaidi ya wanachama 540 wa kijamii wamejiunga kwenye vita dhidi ya ukeketaji na kuanza kulinda wasichana.

Vikundi pia vimebuniwa kuendeleza uhamasishaji dhidi ya maovu hayo.

Alale, wakazi pia wamefungua barabara ya kilomita 13 ili eneo hilo liweze kuingilika kwa urahisi.

Meneja World Vision Kenya, Kaunti ya Pokot Magharibi Tom Masinde anasema mfumo wa Community Change umesaidia kwa kiwango kikubwa kuangazia ukeketaji, ndoa za mepema, unyanyapaa dhidi ya makundi yasiyojiweza, mila na tamaduni potovu.

Hatua zingine ambazo shirika hilo limepiga ni, usawa na haki kwa wote kwenye maboma, kupunguza mapigano ya kijamii, kupigana na vita dhidi ya dhuluma za kijinsia na watoto.

“Wakeketaji wawili wameasi kazi hiyo eneo la Alale. Desemba 2022, hakuna kisa cha ukeketaji kiliripotiwa,” Masinde anasema.

Aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa wakazi hukutana mara tatu kwa wiki, ili kujadili uimarishaji mikakati kupambana na ukeketaji na maovu mengine yanayolengwa.

“Wao hukutana, na kujitambulisha kupitia makundi. Hupitia majukwaa hayo kuweka wazi changamoto wanazopitia na kusaka suluhu,” alisema.

Akielezea imani yake kwa mfumo wa Community Change kugeuza jamii ya Pokot Magharibi, Masinde alisema umeanza kuzaa matunda kwani wanawake sasa wamefunguka na kufichua vya vya ‘kupashwa tohara’.

Isitoshe, wanatumia makundi kujiimarisha kifedha, kimapato na kimaendeleo.

“Kwa sasa wanakusanya na kukopa fedha ili kusaidia watoto shuleni,” alisema.

Oparesheni ya makundi vile vile inashirikisha usafi wa mazingira.

“Maboma mengi hayakuwa na vyoo, lakini sasa nusu yake yana ‘vituo hivyo vya kujisaidia’,” alisema, akiongeza kwamba kwenye boma, baadhi ya wakazi wamejenga vyumba vya watoto kusomea.

Afisa Msimamizi wa Kiutawala Tarafa ya Alale, Maurice Ogweno, anathibitisha visa vya ukeketaji kupungua eneo hilo.

“Ni kisa kimoja tu cha ukeketaji kiliripotiwa 2023 na mhusika amekamatwa,” alisema Bw Ogweno.

Kando na uhamasishaji kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali, afisa huyo alitaja mikutano ya mara kwa mara inayoandaliwa na wazee wa kijiji kusaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na visa vya ukeketaji.

  • Tags

You can share this post!

Wizi: Madereva wa matrela wanavyolazimika kulala mvunguni...

KCSE 2023 yaanza usalama ukiimarishwa vituo vya kufanya...

T L