• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mkuu wa Bandari Lamu atoa sababu ya meli ya watalii kufunga gati sehemu isiyofaa

Mkuu wa Bandari Lamu atoa sababu ya meli ya watalii kufunga gati sehemu isiyofaa

NA KALUME KAZUNGU

MENEJA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (KPA) anayesimamia Bandari ya Lamu, Mhandisi Vincent Sidai ameeleza sababu za meli iliyobeba watalii ya MV SH Diana kutia nanga eneo tofauti na Bandari ya Lamu mnamo Ijumaa.

Jumla ya watalii 57 kutoka nchi za Brazil, Ufaransa, Italia, Marekani, Uingereza, na sehemu nyingine za ulimwengu waliwasili kisiwani Lamu wakiwa wameabiri Meli ya MV SH Diana, ambayo ilitia nanga kwenye jeti ya KPA mjini Lamu.

Watalii hao walilakiwa kwa mbwembwe zilizojumuisha Ngoma za kitamaduni, nyimbo za Taarab, mashairi na tumbuizo nyingine nyingi.

Pia wakikaribishwa kwa kinywaji cha madafu.

Gavana wa Lamu, Issa Abdallah Timamy, Waziri wa Utalii,kaunti ya Lamu Bi Aisha Miraji, Meneja wa KPA katika Bandari ya Lamu, Mhandisi Vincent Sidai Na wakuu wengine walifika kwenye jeti ya KPA kisiwani Lamu kuwalaki watalii hao Na meli yao ya MV SH Diana.

Hii Ni meli ya pili ya kubeba watalii kupokelewa kisiwani Lamu,ya kwanza ikiwahi kufika eneo hilo 2014.
Akizungumza na Taifa Leo muda mfupi baada ya kuwasili kwa Meli hiyo,Be Sidai alisema sababu zilizopelekea meli kutia nanga kwenye jeti ya KPA kisiwani Lamu badala ya Bandarini Lamu huko Kililana ni kutokana Na mkanganyiko Wa mawasiliano kati ya ajenti husika wa meli hiyo na nahodha pamoja na mabaharia.

Kulingana na Bw Sidai, Bandari ya Lamu tayari imeorodheshwa kwenye ramani ya ulimwengu kama miongoni mwa sehemu za kupokea meli za kubeba watalii.

Alipinga kauli ya awali kwamba bandari hiyo haikuwa imeorodheshwa kwenye ramani ya kuruhusu kupokea meli za kubeba watalii ulimwenguni ambazo huchukuliwa sawasawa Na hoteli zinazotembea.

“Twashukuru kupokea meli ya kubeba watalii hapa kisiwani Lamu leo Ijumaa. Bila shaka kuna wanaojiuliza kwa nini meli hii ikatia nanga kwenye jeti ya KPA mjini Lamu badala ya eneo kunakostahili,ambalo ni Bandarini Lamu kule Kililana. Haya yote yanatokana na mkorogeko wa mawasiliano kati ya ajenti Wa meli hii ya MV SH Diana na nahodha. Awali meli ilikuwa imeandaliwa kutia nanga bandarini Lamu lakini akenti akawa baadaye amemwelekeza nahodha kutia nanga hapa jeti ya KPA Lamu. Twatarajia Meli zijazo za watalii zitapokelewa Bandarini Lamu huko Kililana kwani Bandari yetu tayari imesajiliwa kwenye ramani ulimwenguni kwamba itekeleze huduma za kupokea meli za kubeba watalii kutoka pande zote za dunia. Nyote mnakaribishwa,” akasema Bw Sidai.

Wenye mahoteli na maafisa wa sekta ya Utalii Lamu walipongeza ujio wa meli hiyo ya kubeba watalii kisiwani Lamu Ijumaa.Mwenyekiti wa Bodi ya Watalii kaunti ya Lamu (LTA), Ghalib Alwy alitaja ujio huo wa MV SH Diana kuwa baraka tele kwao.

Meli ya watalii kufika hapa Lamu leo ni baraka tosha kwetu. Ni dalili kwamba watalii wako.na imani na Lamu. Lamu Ni salama. Amu ni tamu. Twawakaribisha mfike Lamu kujivunjari,” akasema Bw Alwy.

Mbali ya MV SH Diana,meli nyingine zaidi za watalii zinatarajiwa kuwasili Lamu kati ya Novemba 24 na Desemba 9 mwaka huu, huku mikakati kabambe ya kuhakikisha zinatia nanga eneo la Bandari ya Lamu huko Kililana,Lamu Magharibi ikiendelea.
Bandari ya Lamu ambayo iligharimu serikali kuu kima cha karibu Sh310 bilioni kujengwa ilifunguliwa rasmi kuanza shughuli za uchukuzi mnamo Mei 20,2021.
Hii ni baada ya ujenzi wa viegesho vitatu vya mizigo bandarini humo kukamilika.
Ilifunguliwa na Rais Mstaafu,Uhuru Kenyatta, ambapo siku hiyo kulishuhudiwa Meli ya Kwanza ya MV CAP Carmel kutoka nchini Singapore ikitia nanga kwa mara ya kwanza bandarini humo.

Kufikia sasa jumla ya meli 45 zimetua nanga bandarini Lamu tangu kufunguliwa kwake.

  • Tags

You can share this post!

Mademu, hakikisheni mnazaa na wanaume walio na akili,...

Vizuizi vya polisi vingali barabarani licha ya marufuku ya...

T L