• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Mlo wavuta wengi kujisajili kuwa wapigakura Bondeni

Mlo wavuta wengi kujisajili kuwa wapigakura Bondeni

Na RICHARD MAOSI

WAKAZI wa mtaa wa Bondeni katika Kaunti ya Nakuru, siku ya Jumapili walifurahia mapochopocho ya bure, ikiwa ni njia mojawapo ya kuwavutia wajiandikishe wawe wapigakura, taifa linapojiandaa kushiriki uchaguzi mkuu ifikapo mwaka 2022.

Hafla hiyo ambayo ilibatizwa jina la ‘Chapati Forum’, iliwaleta pamoja vijana, wazee watoto na akinamama, kufurahia vitafunio wengine wakibeba wali kwenye mikoba. .

Kabla ya kupakuliwa msosi, kila mmoja alihitajika kuwa na kitambulisho na cheti cha kuonyesha alikuwa ni mpigaji kura, huku zikisalia siku mbili kabla ya zoezi hilo kukamilika.

“Leo ni kama Krismasi imekuja mapema, nilifika hapa asubuhi na mapema na wala sikuwa na haraka ya kujiandikisha kama mpigakura kwa sababu nilikuwa na uhakika nitapata chakula cha mchana,” akasema Titus Bodo mkazi wa Bondeni.

Alieleza kuwa vijana wengi wamekuwa wakijitenga na shughuli ya kujiandikisha kama wapigaji kura, kwani viongozi hawajakua wakiangazia maslahi yao ya tumbo kwanza.

Pili hawajakuwa wakipata elimu kila wakati nchi inapokaribia kufanya uchaguzi.

Bodo alisema kuwa mwaka 2022 ni lazima atapiga kura ili kuchagua viongozi ambao wataleta maendeleo kwenye mtaa wa mabanda wa Bondeni.

Isitoshe, aliwashauri viongozi kutoka kaunti nyinginezo kuiga mfumo huu, ikiwa wanalenga kufikisha idadi ya wapigaji kura milioni sita kufikia mwisho wa shughuli hiyo.

Alieleza kuwa wakazi wengi hawajakuwa wakipata muda wa kujiandikisha kama wapigakura kwa sababu wamebanwa na kazi, wakitafuta riziki ya kila siku.

Mwandalizi wa hafla hiyo, Bw Kinyanjui Koimbori, aliambia Taifa Leo ameamua kutumia chakula kama chambo ili kuwahamasisha wanaofuzu kuwa wapigakura, kuhusu haki yao ya kimsingi ya kupiga kura.

Aliwasuta wagombea ambao wamekuwa wakionekana mitaani wakati wa kutafuta kura na kutoweka mara tu baada ya kuingia mamlakani.

“Ninawahimiza wakazi waendelee kujiandikisha kama wapigaji kura, ili waweze kuwateua viongozi ambao watayaangalia maslahi yao siku za mbeleni,” akasema.

Hili linajiri siku chache baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kueleza kuwa ni asilimia 13 ya raia ambao wamejiandikisha kama wapigakura.

You can share this post!

Pendekezo la mchujo wa ODM laibua hofu

Wahitimu 1,725 wa Thika Technical washauriwa watumie ujuzi...

T L