• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
Pendekezo la mchujo wa ODM laibua hofu

Pendekezo la mchujo wa ODM laibua hofu

Na WAANDISHI WETU

WAWANIAJI wanaolenga kuwania kiti cha ugavana katika eneo la Nyanza, wameingiwa na hofu kutokana na pendekezo la wajumbe kutumika kuwachagua wagombeaji wakati wa mchujo kuelekea kura ya 2022.

Wiki jana, Naibu Kiongozi wa ODM, Bw Wycliffe Oparanya, alifichua kuwa huenda wakapokeza viongozi tiketi za moja kwa moja, tamko ambalo limeibua mjadala kuwa wapigakura hawatajitokeza katika ngome za Bw Odinga.

Katika Kaunti ya Kisumu, Seneta Fred Outa amepinga vikali pendekezo hilo, akisema itaenda kinyume cha demokrasia ya chama.

“ODM haina budi ila kufanya uteuzi kwa njia huru, haki na uwazi ili kuibuka na viongozi ambao wanawajibikia raia vyema. Hapa Kisumu, watu wachache hawawezi kuketi na kuamua kwa niaba ya wakazi kuhusu nani anayefaa kuwa gavana 2022,” akasema Bw Outa.

Seneta huyo analenga kumpinga gavana wa sasa Profesa Anyang’ Nyong’o 2022 licha ya wawili hao kushirikiana 2017 na kufanikiwa kumbandua aliyekuwa gavana wa kwanza, Bw Jack Ranguma mnamo 2017.

“Kuwapa baadhi ya wanasiasa tiketi ya moja kwa moja kutawazuia wengi kupiga kura hasa wakati huu ambapo Raila yupo pazuri kutwaa uongozi wa nchi,” akaongeza.

Bw Outa ambaye alihudumu kama mbunge wa Nyando kwa mihula miwili kabla ya kuwa seneta, alionekana kukerwa na hatua ya baadhi ya wanasiasa kujinadi kuwa wao wanapendelewa na chama.

“Kauli zao tayari zimesababisha raia kutochamgamkia usajili wa wapigakura unaoendelea kwa kuwa wengi wanasema kura zao hazitathaminiwa iwapo ODM ishawachagulia viongozi.”

Hata hivyo, Mwenyekiti wa ODM Kaunti ya Kisumu, Prof Ayiecho Olweny, alisema kuwa katiba ya chama inaruhusu wawaniaji kuwapa tiketi viongozi maarufu na hata uteuzi kupitia wajumbe.

Katika Kaunti jirani ya Homa Bay, tayari kivumbi kikali cha ugavana kimeanza kushuhudiwa kati ya mwenyekiti wa ODM, Bw John Mbadi, Mbunge Mwakilishi wa Kike, Bi Gladys Wanga na aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Dkt Evans Kidero.

Mbunge wa Dagoretti Kusini, Bw Simba Arati japo alisema pendekezo hilo ni zuri, alidai huenda likasababisha ghasia na kuchangia chama kuwapoteza viongozi maarufu.

Bw Arati anayelenga kiti cha ugavana Kisii, alisema huenda baadhi ya wawaniaji wakawahonga wajumbe wawapigie kura na chama kuishia kupoteza viongozi wazuri.

You can share this post!

TAHARIRI: Kampeni ghali ndizo zinazotuchongea

Mlo wavuta wengi kujisajili kuwa wapigakura Bondeni

T L