• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mwanafunzi mjamzito Nakuru kufanyia KCSE hospitalini

Mwanafunzi mjamzito Nakuru kufanyia KCSE hospitalini

NA JOHN NJOROGE

MWANAFUNZI mwenye ujauzito kutoka eneobunge la Kuresoi Kaskazini, Kaunti ya Nakuru atafanyia jaribio la Somo la Kemia, Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) hospitalini baada ya kulalamikia kulemewa na uchungu.

Mitihani ya Kitaifa ya Kidato cha Nne, KCSE 2023, imeanza leo, Jumatatu, Novemba 6 kote nchini.

Mkurugenzi wa Elimu Kaunti ya Nakuru, Bi Victoria Mulili aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa mwanafunzi huyo alianza kuhisi uchungu na akalazimika kukimbizwa hospitalini.

“Mwanafunzi mwenye ujauzito aliandika mtihani wa Kemia, Karatasi ya Kwanza akiwa hospitalini, kufuatia uchungu aliosema anahisi,” Bi Mulili alisema.

Aidha, alifanya mtihani huo chini ya ulinzi wa askari.

Akizungumza baada ya kusimamia usambazaji wa karatasi za mitihani katika Kaunti Ndogo ya Molo, afisa huyo alisema zoezi hilo lilianza saa moja asubuhi na hakuna changamoto zozote zilizoripotiwa katika siku ya kwanza.

Alisema usalama umeimarishwa ndani na nje ya vituo vya kuandika mtihani.

“Siku ilianza vizuri bila matatizo yoyote na tunatoa wito kwa wasimamizi wa vituo kutojiweka hatarini endapo jambo lolote litatokea katika maeneo yao,” alihimiza.

Kufuatia mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa maeneo mbalimbali nchini, Bi Mulili alisema sehemu ambazo barabara ni mbovu kusafirisha mitihani serikali itatumia njia mbadala kuhakikisha kuwa haichelewi kufika shuleni.

Kila kituo cha mitihani kina afisa wawili wa usalama.

 

  • Tags

You can share this post!

Mzozo wa uongozi wa maskwota katika shamba linalodaiwa...

Pokot Magharibi KCSE yaendelea vyema maeneo hatari usalama...

T L