• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Siri ya kujinasia wateja ni majina tamutamu ya boti

Siri ya kujinasia wateja ni majina tamutamu ya boti

NA KALUME KAZUNGU

MANAHODHA na wamiliki wa boti katika Kaunti ya Lamu wanatumia mbinu mbadala ya kuwavutia wateja kukodi vyombo vyao vya usafiri, ikiwemo kupitia kuvipa vyombo vyao majina yenye mnato.

Haya yanatokana na upinzani mkali unaoshuhudiwa kwenye sekta ya uchukuzi wa majini miaka ya hivi karibuni kwani idadi ya wanaohudumu ndani ya sekta hiyo inaongezeka kila kuchao.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwepo kwa majina mengi yenye mvuto katika vyombo hivyo vya usafiri.

Wamiliki wa vyombo hivyo pia wamejikaza kuweka boti na mashua zao katika hali safi na kudhibiti upya wa vyombo hivyo.

Miongoni mwa majina ya mnato yanayobandikwa botini au mashuani kuvutia wasafiri ni; Mapenzi, Huba, Nuru, Hurulaini, Darling, Malkia, na Malaika.

Wamiliki wa boti na mashua Lamu wameibuka na mbinu mpya ya kuvutia abiria, ikiwemo kuchagua majina murwa kwenye vyombo vyao. PICHA | KALUME KAZUNGU

Baadhi ya manahodha waliohojiwa na Taifa Leo walisema waliafikia kujikaza kuchagua kwa umakinifu majina ya boti au mashua zao, wakishikilia kuwa jina la kuvutia hufaulisha biashara zao.

Hussein Twalib alikiri kuwa mara nyingi mteja huangalia tu jina lililoko kwenye boti au mashua na punde anapovutiwa nalo, huwa hana budi ila kukodi boti husika.

“Mimi ni nahodha ninayehudumia safari za kisiwa cha Lamu na Shella. Tangu nilipochagua jina la mnato na kuweka kwenye boti yangu ambalo ni ‘Mpanezi’, biashara imenoga. Sikosi kuhudumia zaidi ya wateja 100 kwa siku na hiyo ni pesa nzuri,” akasema Bw Twalib.

Omar Abdallah ambaye ni nahodha anayehudumia kisiwa cha Lamu kuelekea kisiwa cha Matondoni anasema wateja wengi, hasa watalii, huvutiwa kukodisha boti zenye majina murwa na ambazo ni safi.

Bw Abdallah anasema awali boti yake alikuwa ameibandika jina ‘Hasira’ hali anayokiri kumgharimu wateja ambao walikuwa wakiikwepa bila ya yeye kufahamu sababu.

Kulingana na Bw Abdallah, wateja wake walikuwa wakitazama tu boti na punde wanaposoma jina ‘Hasira’ waliishia kuiacha boti hiyo na kukodisha nyingine yenye jina la kuvutia likitamkika.

Mwishowe aliafikia kugeuza jina la boti yake ambapo kwa sasa ameibandika jina ‘Cinderella.’

“Nilipogundua kuwa jina hilo linanigharibu biashara yangu, sikuchelewa kuchagua jina mbadala. Boti yangu kwa sasa inaitwa ‘Cinderella’ na sijuti kwani wateja ni kibao siku hizi,” akasema Bw Abdallah.

Ahmed Ali ambaye ni mtengenezaji mashua na boti kisiwani Shella, anataja mbandiko wa majina kwenye vyombo vya usafiri kuwa ‘tasnia’ nzima inayohitaji ubunifu wa hali ya juu.

Bw Ali anasema mbali na majina ya kifahari au ya kimapenzi yanayobandikwa kwenye vyombo vya baharini kuwateka nyoyo wateja kwa macho tu, pia kuna wale ambao hupanda boti kulingana na ushujaa unaodhihirishwa na chombo husika.

Bw Ali anasema boti zenye majina kama vile ‘Samaki Mkuu, Papa, Nyangumi, Nyambizi, na mengineyo hupendwa sana na wateja wengi, wakijua fika kuwa wameabiri chombo chenye nguvu ya kustahimili mawimbi na dhoruba nyingine baharini.

“Sisi wasanii tunaotengeneza hizi boti na mashua tumejua siri. Hatuandiki majina vivi hivi tu kwenye chombo. Lazima tujadiliane na kuafikiana kabla ya kubandika jina chomboni. Kwa mfano, ukipeana jina la ‘Samaki Mkuu’ kwa chombo chochote kile, uwe na uhakika kuwa wateja watavutiwa na boti au mashua hiyo. Samaki Mkuu sifa zake ni ufalme baharini. Kwamba hawezi kushindwa na mawimbi au zahma zingine za baharini. Kumaanisha sifa hizo ndizo zinazooanishwa na chombo chako. Abiria watakodi chombo chako wakijua fika kuwa safari zao zitakuwa salama salmini,” akasema Bw Ali.

Lucy Atieno, mmoja wa abiria na mtalii wa ndani kwa ndani aliyehojiwa na Taifa Leo, alikiri kuwa yeye huwa haabiri mashua au boti yoyote kila anapozuru visiwa vya Lamu. Bi Atieno anasema maamuzi yake ya boti anayopanda kujivinjari baharini mara nyingi huchochewa na uzuri wa boti au mashua na pia jina la chombo husika.

“Ilmradi boti au mashua ina jina zuri, ni safi kwa ndani na nje, ikon a jaketi-salama ambazo ni safi na pia viti vya kukalia viko  hali shwari, mimi hukimbilia boti hizo. Napenda sana vile boti na mashua za Lamu zinavyobandikwa majina mazuri na yenye kuvutia na kuuburudisha moyo na nafsi si haba,” akasema Bi Atieno.

Kaunti ya Lamu ina zaidi ya wahudumu 5,000 wa uchukuzi wa baharini ambao hupatikana kwenye visiwa mbalimbali vya kaunti hiyo.

Miongoni mwa maeneo ya Lamu ambapo uchukuzi mwingi hutekelezwa kwa njia ya bahari ni Lamu, Shella, Manda, Kipungani, Matondoni, Kiwayu, Mtangawanda, Kizingitini, Pate, Siyu, Faza, Mkokoni, Ndau, Kiunga na viungani mwake.

  • Tags

You can share this post!

Ivy Nyangara afuata nyayo za Lupita Nyong’o

Polisi atapika baada ya kunusa vidole vya mshukiwa wa bangi

T L