• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Wanabodaboda Thika wahimizwa kuweka akiba kwa vikundi

Wanabodaboda Thika wahimizwa kuweka akiba kwa vikundi

Na LAWRENCE ONGARO

WANABODABODA wameshauriwa kujisajili rasmi ili waweze kutambulika.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, aliwataka wanabodaboda kuwa mstari wa mbele kuonyesha nidhamu wanapotekeleza majukumu yao ya kuhudumia wananchi.

Alipongeza pendekezo la Inspekta Jenerali wa Polisi, Hilary Mutyambai kwamba wanabodaboda wanafaa kujisajili rasmi ili wajulikane popote walipo.

“Pendekezo lililotolewa hivi majuzi na Inspekta Jenerali wa Polisi kuhusu kujisajili kwa wanabodaboda ni muhimu sana kwa sababu wahudumu hao watajichunga wenyewe kwa kuonyesha nidhamu,” alisema Bw Wainaina.

Aliyasema hayo eneo la Ngoliba, Thika Mashariki alipohamasisha vikundi 130 vya wanabodaboda kutoka Thika.

Idadi ya wanachama katika vikundi hivyo ni 4,000 katika eneo la Thika.

Aliwahamasisha kuhusu umuhimu wa kujiunga kwa vikundi vya watu kumi na zaidi ili kunufaika na mikopo kupitia kwa J-Hela.

Alieleza kuwa iwapo kila mmoja ataweka kwenye akiba Sh100 akiwa katika kikundi bila shaka hata mwaka mmoja watapata zaidi ya Sh1 milioni.

“Mimi ningetaka kuona mhudumu wa bodaboda anatoka katika kiwango hicho na kujinunulia gari lake. Pia ningetaka kuona kila mmoja akijitegemea kibinafsi,” alifafanua mbunge huyo.

Mbunge huyo aliwaahidi kuwa atawapa mikopo kupitia J-Hela punde tu vikundi hivyo vitakapokuwa vimeweka akiba kiwango kinachoambatana na kiwango kinachostahili.

Bw John Mwangi, mhudumu wa bodaboda eneo la Thika, alipongeza jinsi walivyohamasishwa kuhusu kuweka akiba ili kujiendeleza kimaisha.

“Sisi kama wanabodaboda tumekuwa hatuna maarifa ya kuweka akiba lakini wakati huu tumepata mwongozo utakaotupatia mwelekeo bora. Tukitoka hapa ni lazima tujipange kwa vikundi ili tuanze kuweka akiba polepole,” alisema Bw Mwangi.

Alisema wanabodaboda ni watu wenye familia na kwa hivyo ni vyema kuwa na mwelekeo bora wa kimaisha.

Bw Martin Maina, mhudumu mwingine wa bodaboda, alisema, hamasisho walilopata kutoka kwa Bw Wainaina ni muhimu sana kwao kwa sababu limewafungua macho.

“Iwapo tutafuata mwelekeo tuliopewa na mbunge wetu bila shaka maisha ya wanabodaboda yatabadilika pakubwa. Hili ni jambo tutakalozingatia mara moja bila kuchelewa,” alisema Bw Maina.

Wanabodaboda hao walisema baada ya kupata mawaidha ya kuridhisha kutoka kwa mbunge huyo watabadilisha mwelekeo wa maisha yao ili nao waweze kuishi maisha ya kuridhisha kama watu wengine.

  • Tags

You can share this post!

UDAKU: Ya Balotelli na Messina yatibuka!

Watu 31 waliotoweka 2021 bado haijulikani waliko –...

T L