• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Wanaume ‘deadbeat’ Lamu wanaotaliki wake na kutelekeza watoto wafokewa

Wanaume ‘deadbeat’ Lamu wanaotaliki wake na kutelekeza watoto wafokewa

NA KALUME KAZUNGU

MAAFISA wa Idara ya Elimu, kaunti ya Lamu wamewafokea akina baba waliotaliki wake zao kwa kugeuka wakorofi na kuwanyima haki watoto wao.

Wakizungumza kwenye kongamano lililowaleta pamoja wanasheria, mashirika mbalimbali ya kijamii, wanawake kwa wanaume kisiwani Lamu, maafisa hao, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Elimu wa Lamu ya Kati, Bi Rukia Abdallah, walisema mababa punde wanapokosana na wake zao na kutalakiana, wao hudinda kutoa vitambulisho vyao kuwasaidia wana wao kupata hati za kuzaliwa na mahitaji mengine ya maisha.

Kulingana na Bi Abdallah, miongoni mwa matakwa muhimu ya wanafunzi kusajiliwa shuleni kusoma ni kuwepo kwa hati ya kuzaliwa pamoja na vitambulisho vya wazazi wake wawili.

Stakabadhi hizo humwezesha mwanafunzi kujisajili na kupata nambari maalum ya kuhifadhi taarifa za kielimu kumhusu mwanafunzi husika (NEMIS Code).

Bi Abdallah alisema inasikitisha kuona wanafunzi wengi, hasa kisiwani Lamu wakihangaika wakati wa kujisajili shuleni kwani punde baba anapoachana na mama ya mwanafunzi husika yeye hudinda kabisa kushirikiana na akina mama na kukubali stakab adhi zao zitumiwe kufaulisha elimu ya watoto wao.

“Utapata punde mama na baba wanapotalakiana, watoto ndio huumia. Tumekuwa na kesi nyingi za watoto kukosa hati za kuzaliwa, hivyo kuwa vigumu kwa watoto hawa kusajiliwa na kupewa kodi ya NEMIS. Isitoshe, ni vigumu kwa watoto hawa wasio na stakabadhi kama vitambulisho vya wazazi wawili au hati za kuzaliwa kusajiliwa kunufaika na bima ya afya kwa wanafunzi (Supa Cover),” akasema Bi Abdallah.

Aliwasihi wazazi Lamu kujiepusha na migogoro ya kinyumbani na kujizuia kutalakiana, akishikilia kuwa punde hilo linapofanyika watoto ndio huumia.

“Watoto wengi wa wazazi waliotalakiana huwa nidhamu yao ni ya hatihati. Utapata watoto hao mwishowe wanaacha masomo kwa kukosa malezi kamili. Talaka hutatiza wengi, hasa watoto, kwani familia isiyo kamili huwafanya watoto kulelewa isivyo kikamilifu. Tuepuke kutalakiana,” akasema Bi Abdallah.

Kwa upande wake, Mwanaharakati wa Kijamii Kaunti ya Lamu Mohamed Skanda alieleza kutamaushwa kwake na jinsi talaka zinavyowasukuma vijana wengi kujiingiza kwa uhalifu na hata kuishia kushtakiwa, kuhukumiwa na kufungwa jela.

“Inasikitisha kwamba kesi nyingi zinazowasilishwa mahakamani za uhalifu zinajumuisha vijana ambao wazazi wao waliachana. Kati ya watu watano wahalifu, utapata watatu ni wale wa mzazi mmoja baada ya wanandoa kutalikiana. Lazima tuheshimu ndoa na kupokea ushauri mwafaka utakaosaidia hizi talaka kusitishwa kwani madhara yake ni makubwa kwa watoto,” akasema Bw Skanda.

Hata hivyo wanaume na wanawake waliohudhuria kongamano hilo walitofautiana kuhusiana na suala la talaka kuathiri watoto.

Kwa upande wao, wanaume walidai wengi wao wamejaribu kuheshimu na kujenga mkabala mzuri na wanawake wanaowataliki lakini baadhi ya wanawake hao huwa wagumu.

“Sisi akina baba si kwamba tunaamka tu na kudinda kushirikiana kulea watoto licha ya kutalakiana na wake zetu. Ni hawa hawa wenzetu ambao huleta ukorofi unaoudhi hadi kumsukuma mwanamke kuchukia kabisa na kuacha kushirikiana na mke kumlea mwana. Wenzetu wa jinsia ya kike wakibadili tabia tutaishi vyema, raha mustarehe,” akasema Bw Ali Famau.

Nao akina mama walijitetea kuwa licha ya kujaribu njia zote kupata usaidizi kutoka kwa waume wanaotalakiana nao, mara nyingi imeshinikana kwani hao hao wanaume hupenda kushirikiana kumlea mtoto kwa masharti.

“Wengine eti hutaka endapo mtaendelea kushirikiana kimalezi ya mtoto basi mtoto huyo wawe naye. Wewe mama eti ubaki tu kumtembelea mtoto. Wengine hata hutaka mwendelee kushiriki mapenzi licha ya kuachana kama mojawapo ya vigezo vya wao kushirikiana kimalezi ya mtoto. Hilo haliwezekani,” akasema Bi Khadija Ahmed.

  • Tags

You can share this post!

‘Mume wangu analea watoto wetu watatu, lakini hajui...

Maafisa waliokuwa mstari wa mbele Shakahola wakiri safari...

T L