• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
‘Mume wangu analea watoto wetu watatu, lakini hajui wawili si wake’

‘Mume wangu analea watoto wetu watatu, lakini hajui wawili si wake’

NA FRIDAH OKACHI

ULIPIZAJI kisasi umechangia baadhi ya wanaume kulea watoto ambao si wao.

Mume wa Kate anawalea watoto wawili bila kujua kuwa si wake.

Kate hababaiki iwapo mumewe atafahamu alichofanya, kwa sababu mwanamume huyo analea watoto wawili ambao si wake. Kati ya watoto watatu, mmoja ndiye wa mumewe.

Sababu ya Kate kuenda nje ya ndoa ni kulipiza kisasi baada ya mumewe kupata mtoto nje ya uhusiano wao.

“Siwezi nikamwambia ukweli. Mimi mwenyewe ninajua hawa watoto si wake. Alinitesa tukiwa kwenye mahusiano ya ujana. Ni miaka 12 tukiishi pamoja,” alisema Kate.

Mama huyo aliambia Taifa Leo kwamba, mwanzo ndoa yao ilikuwa na misukosuko japo kwa sasa hali iko shwari.

“Tunaishi pamoja nikiwa bado nina machungu. Sielewi mbona alinifanyia hivyo? Naishi na roho ambayo siwezi nikamsamehe licha ya kwamba mimi nimezaa wawili nje,” aliendelea.

Naye Jacob ambaye ni mkazi wa Nairobi, amesalia kubaki bila mtoto. Anaishi na ukweli mchungu baada ya kufahamu watoto wanne aliokuwa akilea si wake.

Mtaalamu huyo wa dawa, alichukua hatua ya kufanya vipimo vya DNA bila kumhusisha mkewe baada ya kupata jumbe za mwanamume mwingine aliyetaka kujua mahitaji ya wanawe kwenye simu ya mkewe.

“Tukiwa kwa ndoa tulizoea kuangalia simu ya mwingine bila vikwazo. Niliamka usiku wa manane nikapata mwanamme mwingine akitaka mke wangu ampe bajeti ya matumizi ya watoto. Iliniumiza sana. Nilianza kufuatilia jumbe zao kila siku. Ulifika wakati nikawa na shauku kuwa wale wana si wangu wote,” alisimulia Jacob.

Baada ya kupata matokeo ya DNA alimueleza dadaye ambaye alimhimiza kuondoka kwenye ndoa hiyo bila kuhusisha aliyekuwa mkewe.

“Niliondoka bila kumpa taarifa zozote, kufikia sasa watoto walimwambia niliwapeleka kufanyiwa vipimo… baada ya matokeo niliondoka na kumuacha,” aliendelea.

Mfamasia huyo alisema anaumizwa kufahamu ukweli na kupoteza miaka 15. Hata hivyo, kimaadili si sahihi kufanya vipimo vya DNA bila makubaliano baina ya pande zote mbili.

“Saa hii naendelea na kazi nikiogopa kutafuta mke wa kuishi naye. Sitaki msukumo wa familia tena kuniambia nitafute mke ambaye atazaa nje ya ndoa. Kazi yangu ndio mke wangu kwa sasa,” alisema Jacob.

Dadaye Jacob, akiwa ameshika stakabadhi zinazoonyesha matokeo ya DNA alisema hatua ya kakaye kufanya uamuzi huo anaiona kuwa ni ujasiri.

“Nilimpenda shemeji sana lakini kitendo alichofanya si kizuri kwa sababu alimpotezea ndugu yangu muda. Heri angemwambia hampendi lakini si kumfanyia vile,” alisema.

Mwanasaikolojia Jane Ngatia, anasema kulipiza kisasi kwa mwenzako ni kufanya kosa kwa makusudi fulani.

“Huwezi fanya kitendo kibaya ndipo mfanane na hutaki kumweleza ukweli. Pili, si maadili mema kuchukua pesa za wanaume wengine kulisha watoto ambao wana baba yao. Huo ni wizi ambao unaendelezwa na wanawake,” alisema Bi Ngatia.

Bi Ngatia anasema matukio kama hayo huenda yakaumiza watoto wakijua ukweli kwa kunyimwa haki ya kujua baba mzazi.

Mwanasaikolojia huyo amesema kila mmoja ana haki ya kujua ukweli lakini si kufanya kisirisiri.

“Baba, mama, watoto wana haki. Jacob alichukua hatua ya kutaka kujua ukweli. Kitu alichokosa kufanya ni kutumia sheria ambayo ingemhusisha mama na yule ambaye anadai kuwa baba wa watoto aliokuwa akiwalea,” alikamilisha Bi Ngatia.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi mfanyabiashara alivyojinasua kutoka kwa ‘mchele...

Wanaume ‘deadbeat’ Lamu wanaotaliki wake na...

T L