• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
3 watangaza nia kumrithi Havi LSK

3 watangaza nia kumrithi Havi LSK

Na FRANCIS MUREITHI

MAWAKILI watatu wametangaza azma yao ya kuwania wadhifa wa Urais wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) ili kurithi nafasi hiyo kutoka kwa mshikilizi wa sasa Nelson Havi.

Mabw Omwanza Ombati, Eric Theuri na Benard Ng’etich, wamejitosa ulingoni wakilenga kurithi nafasi hiyo kutoka kwa Bw Havi kwenye uchaguzi utakaoandaliwa mnamo Machi 17.

Bw Havi amejitosa siasani na kujiunga na Chama cha UDA kinachoongozwa na Naibu Rais Dkt William Ruto. Analenga kiti cha ubunge cha Westlands katika uchaguzi mkuu wa Agosti, 2017.

Hata hivyo, muhula wa Bw Havi wa miezi 18 umekuwa ukizingirwa na utata na misukosuko ndani ya LSK ambayo ina zaidi ya mawakili wanachama 17,000 kote nchini.

“Ningependa kuwahakikishia mawakili wote kote nchini kuwa iwapo nitachaguliwa kama Rais wa LSK, nitadhihirisha uongozi bora na kushirikisha maoni ya wote katika kuendeleza chama hiki,” akasema Bw Ombati.

Mwanasheria huyo alisema kuwa rekodi yake kama wakili ni bora zaidi akirejelea huduma za uwakili alizotoa wakati wa kesi iliyowasilishwa kupinga matokeo ya uchaguzi wa 2017. Pia alijishaua akisema ni kutokana na juhudi zake ambapo mawakili waliwekwa kwenye kundi la watu wanaotoa huduma spesheli nchi ilipofungwa mwaka jana baada ya kupanda kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Aliongeza kuwa iwapo atachaguliwa, atahakikisha kuwa mawakili wanafanya kazi yao katika mazingira ya kuridhisha bila vitisho kutoka kwa maafisa wa serikali au maafisa wa polisi.

Bw Theuri ambaye pia ni mwenyekiti wa tawi la LSK Nairobi, alisema malengo yake ni kurejesha chama hicho katika enzi za zamani ambapo kiliheshimiwa na sauti yake ilisikika kuhusu masuala mbalimbali yenye umuhimu kwa taifa.

Kando na hayo, alisema kuwa atashinikiza kubuniwa kwa sera itakayowaruhusu mawakili washirikishwe kwenye majadiliano ya mikataba ya kibiashara kati ya serikali na mataifa ya nje pamoja na mashirika ya kimataifa.

“Nawataka mawakili waketi kwenye vikao vya majadiliano hayo kwa sababu ni sehemu inayoendana na kazi yetu. Hii ni ajenda ambayo nitahakikisha inatimia iwapo nitachaguliwa Rais wa LSK,” akasema Bw Theuri.

Bw Ng’etich pia ametangaza kuwa anamezea mate wadhifa huo.

Wakili huyo ambaye hufanya kazi yake jijini Nakuru, alitangaza azma yake mnamo Ijumaa wiki jana.

“Mara hii Rais wa LSK anafaa atoke nje ya Nairobi na nina imani kuwa natosha kutwaa wadhifa huo,” akasema Bw Ng’etich.

Bw Havi alichaguliwa Rais wa LSK mnamo Februari 28, 2020 baada ya mtangulizi wake Allan Gichuhi kumaliza muhula wake.

Kati ya mawakili maarufu aliowapiku wakati huo ni Harriette Chiggai, Maria Mbeneka na Charles Kanjama.

Hata hivyo, LSK imekuwa ikikumbwa na mgogoro wa ndani kwa ndani kutokana na uhasama kati ya Bw Havi na Afisa Mkuu Mtendaji wa chama hicho Mercy Wambua.

You can share this post!

Simiu, Jeruto watawala mbio za Valencia Ibercaja kilomita 10

Ndimi za sumu huhepa adhabu

T L