• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Afueni kidogo, bei ya mafuta ikishuka Desemba

Afueni kidogo, bei ya mafuta ikishuka Desemba

Na CHARLES WASONGA

WAKENYA wamepata afueni kidogo msimu huu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya baada ya serikali kupunguza bei ya mafuta japo kwa kiwango kidogo.

Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (EPRA) imepunguza bei ya petroli kwa Sh5 kwa lita huku ikishusha bei ya dizeli na mafuta taa kwa Sh2 na Sh4, mtawalia.

Hii ina maana kuwa kuanzia Desemba 15 bei ya petroli itauzwa Sh212.36 kwa lita jijini Nairobi na viunga vyake kutoka bei ya sasa ya Sh217.36.

Nayo dizeli itauzwa kuwa Sh201.47 na mafuta taa ikiuzwa kwa Sh199.05, kutoka bei ya Sh203.47 na Sh203.06, mtawalia.

Bei hizo zitatumika kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi Januari 14, usiku wa manane.

Bei ya bidhaa hizi katika maeneo mengine nchini zitagemea umbali kutoka Mombasa ambako shehena za bidhaa hizo hushuka kutoka ng’ambo.

“Bei hizo mpya zinajumuisha ushuri wa VAT wa kima cha asilimia 16 kulingana na Sheria ya Fedha na Sheria za Ushuru ya 2020. Aidha, zinajumuisha ushuru wa bidhaa uliyoanishwa na mfumko wa bei kulinga na hitaji la notisi ya kisheria nambari 194 ya 2020,” Epra ikasema Alhamisi jioni kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Mamlaka hiyo ilieleza kuwa punguzo hilo la bei ya mafuta linatokana na kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo katika masoko ya kimataifa.

Kwa mfano, kulingana na Epra, bei ya petroli ilipungua kwa kima cha asilimia 16.11 kutoka dola 827.75 za Amerika (Sh125,818) kwa pipa mnamo Oktoba, 2023 hadi dola 694.44 (Sh105,554) mwezi wa Novemba 2023.

Ni kutokana na kupungua huku kwa bei ya bidhaa hizi katika masoko ya kimataifa ambapo juzi kiongozi wa upinzani Raila Odinga aliishinikiza serikali kushusha bei kwa kiwango cha kati ya Sh48 hadi Sh50 kwa lita.

“Tuko na habari kwamba bei ya mafuta kule nje imeshuka kwa kiwango kikubwa zaidi. Kwa hivyo, sisi kama Azimio hatutaki serikali kupunguza bei  Sh5 bali tunataka ipunguze bei kwa hadi Sh50 kwa lita moja,” akasema akiwa kaunti ya Kajiado.

  • Tags

You can share this post!

Nakubali tatizo ni mimi, Akothee asema akirejelea mahusiano...

Vibanda vinavyofuga wahuni na wahalifu Ruiru 

T L