• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
Aliyekuwa kinara wa NHIF Richard Kerich akwepa jela

Aliyekuwa kinara wa NHIF Richard Kerich akwepa jela

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA kinara wa shirika la Bima ya Afya Nchini (NHIF) Richard Kerich pamoja na vigogo wa kampuni ya kutoa huduma za matibabu wameachiliwa huru katika kesi ya kula njama kuifilisi serikali Sh116.9 milioni.

Bw Kerich alikuwa ameshtakiwa kuipa kampuni ya Meridian Medical Centre Limited (MMCL) zabuni ya kutoa huduma za matibabu kwa watumishi wa umma na idara ya jeshi.

Hakimu mkuu katika mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bi Eunice Nyuttu aliwaachilia Kerich, maafisa wa zamani wa NHIF Marwa Fadhili Chacha na David Chingi.

Pia aliwaachilia wakurugenzi wa kampuni ya Meridian Medical Centre Limited (MMCL) Bw Peter Ngunjiri Wambugu na Bw Ndiba Wairioko.

Akiwaachilia washtakiwa hao sita hakimu alisema “upande wa mashtaka ulishindwa kabisa kuthibitisha kesi dhidi ya washtakiwa hawa.”

Hakimu alikashfu wachunguzi na maafisa wakuu serikalini waliokagua matumizi ya fedha za shirika hilo la kitaifa la bima ya afya.

“Nimeshangaa jinsi maafisa wa serikali walivyofikia uamuzi kuhusu uporaji wa Sh116 milioni na Sh43 milioni ilhali utaratibu wa kuhesabu pesa haukufafanuliwa,” alisema Bi Nyuttu.

Hakimu aliwaachilia washtakiwa hao ambao kesi iliyowakabili ilikaa kortini miaka zaidi ya 10.

Upande wa mashtaka uliwaita mashahidi 39.

“Nakubaliana na wakili Stephen Bundotich wa kampuni ya mawakili ya Kale & Maina kwamba hakuna  shahidi hata mmoja kati ya mashahidi 39 aliyejaribu kufafanua kuhusu ufisadi huo,” alisema Bi Nyuttu.

Akiwaachilia washtakiwa hao hakimu alisema: “Baada ya kutathmini ushahidi wote, nimefikia uamuzi kwamba upande wa mashtaka umeshindwa kabisa kuthibitisha kesi dhidi ya washtakiwa. Wote wameachiliwa huru.”

  • Tags

You can share this post!

Mnamuaibisha Raila, kiongozi wa jamii ya Waluo aambia...

Uhuru alihepwa na kuaibishwa na Wazungu aliposhtakiwa...

T L